Home Namungo FC NAMUNGO FC WAWEKA REKODI YA NCHI KWENYE MASHINDANO YA CAF

NAMUNGO FC WAWEKA REKODI YA NCHI KWENYE MASHINDANO YA CAF


HAIJAWAHI kutokea! Namungo imeandika rekodi ambayo haijawahi kuandikwa kwa timu za Tanzania kwenye michuano ya kimataifa kwa kushiriki kwa mara ya kwanza na moja kwa moja kwenda makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika.

Namungo ikishiriki kwa mara ya kwanza Kombe la Shirikisho Afrika msimu huu na wanafikia malengo yao ya kufuzu hatua ya makundi.

Wamefuzu katika hatua hiyo baada ya kuwaondoa CD de Agosto ya Angola kwa jumla ya mabao 7-5, katika michezo yake miwili ambayo yote walicheza katika Uwanja wa Azam Complex, ule wa kwanza ilishinda mabao 6-2 kisha waliporudiana katikati ya wiki ilipoteza 3-1.

Wauaji wa Kusini hao, wameangukia kwenye Kundi D ikiwa na timu za Raja Casablanca ya Morocco, Pyramids ya Misri na Nkana FC ya Zambia na wataanza kazi ikiwa ugenini kuvaana na Raja katika mchezo utakaopigwa Machi 10.

Safari ya Namungo kwenye michuano hiyo ilianza kwa kutinga fainali ya Kombe la Shirikisho (ASFC) na kupoteza mbele ya Simba kwa mabao 2-0 na kiupata tiketi kwa vile Simba ilibeba pia ubingwa wa Ligi Kuu Bara na kuanza kazi dhidi yav Wasudani Kusini na Sudan na kote ikapeta.

Ndipo wakakutana na Primiero de Agosto na kuwang’oa na sasa wapo makundi ikiwa timu ya pili kufika hatua hiyo kutoka Tanzania baada ya Yanga iliyotinga hatua hiyo mwaka 2016 na 2018.

SEY, SABILO WASHINDWE WAO

Katika hatua nyingine washambuliaji wawili wa Namungo, Stephano Sey na Sixtus Sabilo washindwe wenyewe katika mashindano hayo.

Sey na Sabilo wawili hao kila mmoja mpaka wanakwenda katika hatua ya makundi walikuwa ndio vinara wa ufungaji kila mmoja akiwa amefunga mabao matano.

Kama wataweza kukaza na kuendeleza na moto wao huo wa kufunga katika hatua ya makundi wanaweza kutwaa tuzo ya mfungaji bora.

Wawili hao hata kama wakishindwa kutwaa tuzo ya ufungaji bora wanaweza kujitengenezea wasifu ambao unaweza ukawavutia timu nyingine na wakatoa mkwanja mrefu wa kuwasajiki.

WAPINZANI WAO

Namungo baada ya kufuzu katika hatua ya makundi watakutana na wakati mgumu dhidi ya timu tatu ambazo umepangwa kukutana nazo.

Haitakuwa kazi rahisi kwa Namungo kwenda katika hatua inayofuata kwani kundi lake linatimu, Raja Casablanca kutokea Morocco, Nkana Red Devils (Zambia) na matajiri Pyramids kutokea Misri.

Timu hizo tatu ambazo Namungo watakutana nazo kwanza ni wazoefu wa mashandindano ya kimataifa ambayo wao wanacheza kwa mara ya kwanza, lakini bajeti zao katika mambo mbalimbali ya msingi ni kubwa.

Ugumu mwingine ambao Namungo wanakwenda kukutana nao hizo timu zina wachezaji wenye uzoefu wa mashindano na hata bajeti zao katika usajili na posho nyingine ni kubwa.

Katika mpira lolote linaweza kutokea kama Namungo anaweza akafanya maandalizi yake na kupata matokeo mazuri kwenye mechi za nyumbani na hata ugenini anaweza kusonga katika hatua inayofuata.

SOMA NA HII  WAKATI YANGA WAKIUUMA ANA NAMUNGO....LUSAJO ATAENDELEA KULA MKATE MKAVU LEO...?

KUVUTA MAMILIONI

Shirikisho la soka Afrika (CAF), litawapa Namungo zaidi ya Sh600 milioni baada ya kufuzu katika hatua ya makundi kama pesa ya kufanya maandalizi na mambo mengine ya msingi.

Kitita hicho cha pesa kitaanza kuingia katika akaunti zao kabla ya kucheza mechi ya kwanza katika hatua ya makundi ili kujikimu katika kambi, kusafiri, posho za wachezaji na mambo mengine.

Pesa hiyo zaidi ya Sh600 milioni si kama yote itaingia katika akaunti yao kwani Sh100 milioni itakwenda katika Shirikisho la soka Tanzania na huo ni utaratibu ambao umewekwa tangu hapo awali.

Namungo kama watakuwa na matumizi mazuri pesa hiyo inaweza kuwasaidia katika maandalizi na mambo yao mengine yote ya msingi katika mechi zote za hatua ya makundi.

KOCHA AFUNGUKA

Kocha wa Namungo, Hemed Suleiman ‘Morocco’ anasema ni jambo kubwa kwa timu kama yake kufika kwenye hatua ya makundi katika mashindano hayo ambayo kuna ushindani wa kutosha.

Morocco anasema walikuwa na malengo ya kufika hatua hiyo ambayo wameifikia na kazi kubwa imebaki katika hatua ya makundi ambayo wanakutana na timu za maana.

“Ukiangalia timu tatu tulizokuwa nazo katika kundi letu zetu ni wazoefu wa kucheza mashindano haya mara kwa mara kuliko sisi ambao tunacheza kwa mara ya kwanza,” anasema.

“Tutakutana na ushindani pamoja na ugumu wa kutosha kutoka katika maeneo tofauti kutokana na ugeni wetu wa mashindano ila tutafanya maandalizi ya yote hayo ili kuona namna gani tutafanya vizuri.

“Kutokana na hatua tuliyofikia na kikosi changu kilivyo lazima nitapendekeza wachezaji wengine wapya wenye ubora ili kuja kuongeza nguvu,” anasema Morocco.

UONGOZI NAO

Mwenyekiti wa Namungo, Hassan Zidadu anasema mara baada ya kufuzu katika hatua ya makundi maandalizi yao yanaanza haraka zaidi.

Zidadu anasema watakaa na benchi la ufundi kuwasikiliza changamoto na mahitaji yao ili kwa nafasi ya uongozi waweze kuwatimiza na waende katika makundi kwa ajili ya kushindana.

“Kama kutakuwa na masuala ya usajili kwa maana ya kuongeza wachezaji wengine hilo tutawasilikiza benchi la ufundi pamoja na mahitaji yao mengine yote ya msingi,” anasema.

“Hatua tuliyofikia ni kubwa na malengo ambayo tulitamani kuwa nayo kwenye mashindano haya msimu wetu wa kwanza tumeyafikia kazi kubwa imebaki kupambana ili kufika mbele zaidi.

“Timu kama Namungo kufika kwenye hatua ya makundi msimu wake wa kwanza wa mashindano haya si jambo dogo tunastahili pongezi,” anasema.

Katika hatua nyingine Zidadu anasema wataweka nguvu katika ligi kwani hawapo kwenye nafasi nzuri ingawa ndio timu iliyocheza michezo michache.