KOCHA mkuu wa klabu ya Yanga, Cedric Kaze amefunguka kuwa, anaamini kurejea kwa baadhi ya nyota wake muhimu waliokuwa na majeraha kutaisaidia timu hiyo kufanya vizuri na kuibuka na ushindi kwenye mchezo wao wa leo dhidi ya Coastal Union.
Yacouba ambaye hajaichezea Yanga mchezo wowote tangu kuanza kwa mwaka huu kutokana na majeraha ya misuli, tayari amekwisharejea uwanjani na yupo kwenye orodha ya kikosi kitakachocheza dhidi ya Coastal leo.
Yanga inaingia katika mchezo huu ikiwa na kumbukumbu nzuri ya ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Coastal Union, katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliopigwa katika uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam Oktoba 3, mwaka jana.
Akizungumzia kurejea kwa nyota hao, kocha Kaze amesema: “Kwanza siwezi kusema kama tulikuwa tunapata wakati mgumu kusaka matokeo, bali ni changamoto za kiufundi na kukosekana kwa baadhi ya wachezaji wetu muhimu.
“Lakini jambo zuri ni kwamba tayari baadhi ya nyota hao muhimu ikiwemo Yacouba wamerejea, hali hii inanipa matumaini makubwa ya kuamini tutafanya vizuri katika michezo yetu ijayo.
“Tunataka kuanza na mchezo wa kesho (leo) dhidi ya Coastal Union, ambao ni lazima tushinde ili kuendelea kujiimarisha katika uongozi wa ligi,”
Yanga inakamatia usukani wa ligi na pointi zao 49 walizokusanya, baada ya kucheza michezo 21 wakishinda mechi 14 na kutoa sare michezo saba.