Muda mfupi baada ya kutoka sare tasa na Simba leo nyumbani huko Sudan, Al Merrikh imemfukuza kocha wake Nasreddin Nabi na benchi lake lote la ufundi
Nabi ametimuliwa akiwa ameiongoza timu hiyo kwa siku 34 tu tangu alipojiunga nayo Februari 2 mwaka huu akichukua mikoba ya Mserbia Midrag Jesic.
Matokeo hayo ya sare yameiweka Al Merrikh katika nafasi ngumu ya kufuzu hatua ya robo fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu kutokana na msimamo wa kundi hilo ulivyo.
Timu hiyo ili ifuzu robo fainali, inahitajika kuibuka na ushindi katika mechi zake zote tatu zilizobakia za mzunguko wa pili dhidi ya Simba, Al Ahly na AS Vita Club kisha kuombea wapinzani wake hao wafanye vibaya ili yenyewe iweze kufuzu.
Uongozi wa Al Merrikh umeonekana kutofurahishwa na mwenendo wa timu yao jambo ambalo limewashawishi kuachana naye.
Taarifa iliyotolewa kupitia kurasa za mitandao ya kijamii ya klabu hiyo, zimethibitisha kuwa Nabi na wasaidizi wake wamepigwa chini
“Baraza limeamua kuvunja benchi lote la ufundi linaloongozwa na Nabi na wasaidizi wake,” imesema taarifa hiyo.
Nabi ametimuliwa wiki moja baada ya majirani zao Al Hilal kumtimua kocha Zoran Monojlovic baada ya timu hiyo kulazimishwa sare nyumbani na TP Mazembe.
Kabla ya kutoka sare na Simba, Al Merrikh ilipoteza mechi mbili za mwanzo za hatua ya makundi ambazo ilicheza dhidi ya timu za Al Ahly na AS Vita Club.
Ilianza kwa kuchapwa mabao 3-0 ugenini na Al Ahly ya Misri na baada ya hapo wakachapwa mabao 4-1 nyumbani wiki iliyopita