ISMAIL Aden Rage, Mwenyekiti wa zamani wa Klabu ya Simba amesema kuwa ikiwa madai ambayo yanaelezwa kuhusu wachezaji wa Al Merrikh kucheza wakiwa wamefungiwa kucheza mechi kwa miezi sita basi wana kazi ya kufuatilia kwa ukaribu madai hayo.
Kwenye mchezo wao wa Ligi ya Mabingwa Afrika uliochezwa Machi 6, Uwanja wa Al Hilal, dakika 90 zilikamilika kwa Al Merrikh kutoshana nguvu bila kufungana na kugawana pointi mojamoja.
Habari zimeeleza kuwa kuna uwezekano wa Simba kuweza kupewa pointi za mezani ikiwa itabainika ni kweli wachezaji hao walicheza wakiwa na adhabu hiyo.
Imeelezwa kuwa Al Merrikh iliwajumuisha mchezoni wachezaji watatu waliokuwa wamefungiwa kucheza soka kwa miezi sita kutokana na kosa la kusaini mikataba kwenye timu mbili tofauti ambazo ni Al Merrikh na Al Hilal zote za Sudan.
Wachezaji hao ni Mohamed AlRashed, Ramadan Agab na Baljit khamis. Ikiwa Simba inayonolewa na Kocha Mkuu, Dider Gomes itapewa pointi hizo tatu za mezani itafikisha jumla ya pointi 9 na itakuwa inaongoza ligi.
Rage amesema kuwa Klabu ya Simba inapaswa kuwa ili timu hiyo iweze kupata pointi tatu ni lazima ifuatilie kwa umakini suala hilo kuanzia vibali vya wachezaji pamoja na mikataba yao.