ALIYEKUWA kocha mkuu wa kikosi cha klabu ya Yanga, Cedric Kaze amewaambia waajiri wake hao kuwa, kama wanataka kuwa na kikosi bora ni lazima wahakikishe wanafanya usajili wa kuboresha zaidi kikosi hicho kwa kuwa kwa sasa hakijitoshelezi.
Yanga juzi Jumapili ilifikia maamuzi ya kuvunja benchi la ufundi la timu hiyo kutokana na mwenendo mbaya wa timu, ambapo kati ya michezo sita iliyopita ya Ligi Kuu wamefanikiwa kushinda mchezo mmoja pekee.
Mpaka anaonyeshwa mlango wa kutokea juzi usiku, Kaze alikuwa ameiongoza Yanga kwenye jumla ya michezo 25, akishinda michezo 16, amefungwa michezo miwili na kutoa sare mechi saba.
Kati ya michezo hiyo 25, michezo 18 ni ya Ligi Kuu Bara, michezo minne ni ya kombe la Mapinduzi, michezo miwili ya kirafiki na mchezo mmoja ni wa kombe la Shirikisho la Azam maarufu, kombe la FA.
Akizungumzia kufutwa kwake kazi, Kaze amesema: “Tangu nilivyofika Yanga nilisema wazi kuwa miongoni mwa matatizo makubwa tuliyokuwa nayo ni kutokujitosheleza kwa kikosi tulichokuwa nacho.
“Ni kweli viongozi walijitahidi kufanya usajili mzuri mwanzoni mwa msimu, lakini bado hatukuwa na wachezaji wenye daraja bora ambao wanaweza kuziba pengo la mchezaji yeyote anayecheza ndani ya kikosi cha kwanza ‘deep bench’ iwapo anakosekana.
“Hii ndiyo maana majeruhi yalikuwa adui mkubwa kwetu, kwani nyota waliokuja kuchukua nafasi za majeruhi hawakuweza kutupa kile kitu tunachokihitaji.
“Lakini hata dirisha dogo viongozi walijitahidi kusajili lakini kwa bahati mbaya huwezi kubadilisha wachezaji nane kwenye dirisha dogo, lakini ili kuwa bora ni lazima Yanga isajili wachezaji wa kuweza kupambana na nyota wanaoanza kwenye kikosi cha kwanza,”