GEORGE Lwandamina, Kocha Mkuu wa kikosi cha Azam FC amesema kuwa wachezaji wake wapo tayari kwa ajili ya mchezo wao wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Ihefu FC unaotarajiwa kuchezwa Uwanja wa Azam Complex.
Mchezo huo ni wa mzunguko wa pili utapigwa kesho, Machi 11. Mchezo wa kwanza uliochezwa Mbeya, ubao ulisoma Ihefu 0-2 Azam FC.
Lwandamina amesema kuwa anatambua utakuwa na ushindani mkubwa ndani ya uwanja kutokana na vita ya nafasi pamoja na pointi ila anaamini kila kitu kitakuwa sawa.
“Wachezaji wapo sawa na wanatambua kwamba kwa sasa mzunguko wa pili ushindani ni mkubwa hivyo wataingia ndani ya uwanja kusaka ushindi ili kufikia malengo ambayo tumejiwekea,” .
Zuber Katwila, Kocha Mkuu wa Ihefu FC amesema kwamba kikubwa ambacho wanakitazama ni kupata ushindi ndani ya uwanja.
“Tunahitaji ushindi kwenye mechi zetu ili kupata matokeo chanya, ushindani ni mkubwa nasi tunapambana ili kuweza kuwa kwenye ubora wetu,” amesema.
Ihefu FC kwenye msimamo ipo nafasi ya 16 imekusanya jumla ya pointi 20 inakutana na Azam FC ambayo ipo nafasi ya tatu na ina pointi 41.
Kipa namba moja wa Azam FC ni Martin Kigonya huku yule wa Ihefu ni Deogratius Munish, wote ni maingizo mapya kwenye usajili wa dirisha dogo.