ALIYEWAHI kuwa Mwenyekiti wa Klabu ya Simba, Ismail Aden Rage, amesema Yanga walichelewa kufanya maamuzi ya kumfukuza Kocha Cedric Kaze.
Rage aliweka wazi kuwa mipango ya kocha huyo raia wa Burundi ilishafeli, hivyo kama wangeendelea kuwa naye wangekumbwa na dhahama nzito na siku ambayo wangecheza na Simba wangefungwa mabao 7-0.
Akitaja nani anafaa kuwa kocha mpya wa timu hiyo, Rage alifunguka kuwa, Yanga wanatakiwa kutafuta kocha kutoka Ulaya ambaye atakuwa na uwezo kama wa Didier Gomes Da Rosa ambaye tangu ametua Simba mambo yanakwenda vizuri.
Rage amesema:-“Uamuzi wa Yanga kumfuta kazi kocha wao, mimi nauunga mkono mara 100, kwanza walichelewa kufanya maamuzi hayo, yule kocha alionekana kabisa kwamba mipango yake imekataa, kama angeendelea kusalia pale mambo yangekuwa mabaya zaidi na sisi tungewapiga 7-0.
“Kwa sasa wanatakiwa kutafuta kocha Mzungu, kutoka Ulaya kwa sababu wale ndiyo wenye mpira wao. Tazama kocha wa Simba tangu ametua klabuni hapo, mambo yote yanakwenda sawa,” alisema Rage.
Yanga walitangaza kufuta benchi lao lote la ufundi usiku wa Machi 7, mara baada ya kuambulia sare ya 1-1 dhidi ya Polisi Tanzania kwenye mchezo uliochezwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.