UONGOZI wa Yanga umesema kuwa Metacha Mnata bado ni kipa wa timu hiyo licha ya kwamba alifanya maamuzi ya kuaga wachezaji pamoja na uongozi kutokana na presha.
Hivi karibuni Mnata aliamua kuwaaga mashabiki pamoja na viongozi wa Yanga kwa kile kilichoelezwa kuwa alipigwa simu na kiongozi wa timu ambaye ni Mwenyekiti Dr Mshindo Msolla.
Inaelezwa kuwa Msolla alitajwa kumlaumu Mnata kwa kosa la kufungwa mabao ya kizembe jambo ambalo limewafanya wawe wanapoteza pointi tatu.
Bao la dakika ya 89 alilofungwa Mnata mbele ya Polisi Tanzania Machi 7 linatajwa kuwa chanzo cha kupigwa simu jambo lililofanya aweze kuandika ujumbe wa kujiengua ndani ya timu.
Akizungumza kuhusu hilo, Msolla amesema kuwa aliongea na meneja wa Mnata ambaye ni Jemedari Said ili wamalize tofauti ambazo zilikuwepo kati yao.
“Unajua nilishangaa nilipoambiwa kwamba Mnata amepigiwa simu na kiongozi na mimi ninatajwa kumpigia, sina tabia ya kufanya hivyo zaidi huwa ninaongea na meneja wake Jemedari kuhusu maendeleo yake.
“Baada ya kupata taarifa hizo nilimtafuta meneja wake na tukaongea naye na kumaliza zile tofauti ambazo zilikuwepo na ukweli ni kwamba mimi sikumpigia simu ila namba ilionyesha ni yangu naamini kwamba walihack namba yangu,”.