UONGOZI wa Yanga umewaondoa hofu mashabiki wa timu hiyo kwa kuwaambia kuwa kiungo wao mshambuliaji, Mrundi Saidi Ntibazonkiza ‘Saido’ ni mali yao na badala yake kuachana na proganda zinazoendelea.
Hiyo ikiwa siku moja imepita tangu taarifa zienee za kiungo huyo kusaini mkataba wa miaka miwili kuichezea KCCA inayoshiriki Ligi Kuu ya Uganda.
Nyota huyo ambaye yupo nje ya uwanja tangu michuano ya Kombe la Mapinduzi iliyofanyika visiwani Zanzibar Januari, mwaka huu, wiki moja iliyopita aliondoka nchini na kurudi kwao Burundi.
Akizungumza na Spoti Xtra, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa Yanga, Hassani Bumbuli, alisema Saido ni mali yao na juzi alizungumza naye.
Bumbuli alisema kuwa, kiungo huyo amesikitishwa na taarifa hizo ambazo kwake hazijamfurahisha huku akitamani kupona haraka ili arejee uwanjani kuipambania timu yake.
“Mara ya mwisho kuongea na Saido ni Jumatatu kwa njia simu na mimi ndiye niliyempigia, kikubwa ni kutaka kufahamu maendeleo yake akiwa nyumbani kwao Burundi.
“Aliniambia yupo gym, lakini nilizungumza naye kidogo kabla ya kuendelea na mazoezi na kikubwa nilimfahamisha kuhusiana na taarifa hizo, kiukweli alisikitishwa sana,” alisema Bumbuli.
Yanga ipo nafasi ya kwanza kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 50.