Home Namungo FC WAWAKILISHI WA KIMATAIFA KAZI KUBWA YA KUFANYA KUFIKIA MALENGO

WAWAKILISHI WA KIMATAIFA KAZI KUBWA YA KUFANYA KUFIKIA MALENGO


USHINDANI unazidi kukua kila iitwapo leo kwenye mashindano ya kimataifa huku wawakilishi wetu wakizidi kupambana kusaka ushindi. Ni Simba na Namungo ambao wanapeperusha bendera ya Tanzania.

Simba kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika huku wao wanakazi kubwa ya kufanya kufikia malengo yao ambayo wameweka wazi kwamba wanahitaji kutinga hatua ya robo fainali. Namungo wao ni kwenye Kombe la Shirikisho wana kazi kubwa ya kufanya.

Ushindi wa mabao 3-0 walioupata mbele ya Al Merrikh bado sio tiketi kwao kutinga hatua ya robo fainali kwa kuwa ushindani bado unaendelea na wanahitaji kushinda mchezo wao ujao dhidi ya AS Vita.

Kupata ama kukosa ushindi kwenye mchezo ni sehemu ya mpira na kinachotakiwa ni kila mchezaji kuweka akili kwenye mechi zijazo.

Viongozi wa Simba wameweka wazi kwamba wanahitaji kuona timu hiyo ikitinga hatua ya robo fainali. Hatua hiyo haiwezi kuja ikiwa hakutakuwa na mapambano muda wote.

Kinachotakiwa ni kutazama mechi zijazo ili kuweza kurekebisha makosa ambayo yamepita. Ikiwa watashindwa kutazama pale ambapo waliangukia ama kufanikiwa bila kuwa na mipango itakuwa kazi nyingine kufikia mafanikio.

Namungo kazi ya kusaka ushindi mbele ya Pyramids FC ya Misri ilikuwa nzito na mwisho ilikubali kupoteza kw kufungwa mabao 2-0, Uwanja wa Mkapa. Ni mchezo wa pili kwa timu hiyo inayonolewa na Hemed Seleman, ‘Morocco’ kupoteza kwenye Kombe la Shirikisho.

Bado kupoteza mechi mbili haina maana kwamba mapambano yamekwisha ni lazima kazi iendelee kujipanga zaidi.

Mchezo wa kwanza ilipoteza ugenini kwa kufungwa na Raja Casablanca na wa pili pia ikapoteza.

Kwa wachezaji nguvu kubwa itumike katika kuelewa kile ambacho mnafundishwa na kukifanyia kazi ndani ya uwanja. Muda wa maandalizi ni muda pekee wa kurekebisha makosa ambayo mnayafanya ndani ya uwanja.

Msisahau kwamba kuna mawakala ambao wanafuatilia mashindano haya makubwa. Kazi ni kwenu kuwa sokoni kwa wakati huu ambao mnapeperusha bendera ya Tanzania.

Wachezaji pambaneni bila kuchoka ndani ya uwanja ili kuweza kufanya vizuri. Ushindani upo wazi nanyi pia ongezeni juhudi katika kusaka matokeo.

SOMA NA HII  TWIGA STARS YATINGA FAINALI COSAFA

Jambo kubwa la kufanya ni kukubali kujifunza na pale ambapo mnakosea mna kazi ya kurekebishana wenyewe kwa wenyewe ili kusaka matokeo kwenye mechi zenu ambazo mtacheza.

Kila mchezaji anapenda kuona timu inapata matokeo mazuri. Ikiwa morali itakuwa kubwa kwa kila mchezaji itaongeza nguvu pia ya kupata matokeo mazuri wakati ujao kwenye mechi za ushindani.

Bado kazi ni nzito ila itarahisishwa ikiwa kila mchezaji atakubali kujitoa na kutimiza majukumu yake kwa wakati ndani ya dakika 90.

Imani yangu ni kwamba wachezaji mtazidi kupambana kwa ajili ya mechi zote za ushindani kitaifa na kimataifa. Kikubwa ni kuongeza juhudi bila kukata tamaa.

Tukirejea kwenye ligi yetu ya Tanzania ambayo inazidi kuwa na ushindani mambo yanazidi kubadilika kila leo.

Ushindani kwa timu uwanjani ni mkubwa. Pia kila timu imewekeza kiasi cha kutosha ikihitaji kupata matokeo, Jambo la msingi ni kwamba kusiwe na ujanjaujanja kwenye kusaka matokeo.

Ni muda wa wachezaji kufanya vizuri ili kuzipa timu zao matokeo chanya. Hilo litawafanya wazidi kukuza thamani zao sokoni.

Waamuzi jukumu lao ni moja kusimamia sheria 17 za mchezo. Mashabiki nao watimize majukumu ya kushangilia bila ya bugudha.