JUMA Mwambusi, Kaimu Kocha Mkuu wa Yanga amesema kuwa washambuliaji wake wote watarejea kwenye ubora wao na kufanya vizuri kwenye mechi zao zijazo.
Ndani ya Yanga kinara wa utupiaji ni winga, Deus Kaseke huku washambuliaji wake ambao ni Michael Sarpong, Yacouba Songne hawa wametupia mabao manne kila mmoja.
Ditram Nchimbi yeye ana pasi moja ya bao huku Wazir Junior na Fiston Abdulazack wakiwa wametupia bao moja ndani ya kikosi hicho kinachoongoza ligi na pointi 50.
Jumla kimetupia mabao 36 baada ya kucheza mechi 23 kwa msimu wa 2020/21 na Cedrik Kaze ambaye alikuwa kocha mkuu wa timu hiyo alifutwa kazi Machi 7 kwa kile kilichoelezwa kuwa ni mwendo mbovu wa timu.
Kaze aliweka wazi kuwa tatizo kubwa lilikuwa kwenye safu ya ushambuliaji ambayo ilikuwa inasumbuliwa na ubutu jambo ambalo Mwambusi ameweka wazi kwamba anaanza kulifanyia kazi.
Mwambusi amesema:”Maandalizi ya timu yapo kwenye kila sekta ikiwa ni pamoja na suala la ushambuliaji ambalo limekuwa tatizo kubwa kwa wachezaji.
“Nina amini kwamba kupitia mazoezi ambayo tunayafanya kila mmoja atakuwa tayari kuonyesha uwezo wake na atajenga hali ya kujiamini kwenye mechi zetu zijazo,”.