UONGOZI wa KMC umeweka wazi kwamba kesho wataanza maandalizi kwa ajili ya mechi za Ligi Kuu Bara pamoja na Kombe la Shirikisho.
Christina Mwagala, Ofisa Habari wa KMC amesema kuwa wachezaji watarudi kambini kuanza mazoezi rasmi.
KMC walisimamisha mazoezi kwa muda kutokana na kupisha mechi za kimataifa ambapo ilikuwa ni kufuzu Afcon na jana Machi 28, timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars ilimenyana na Libya.
Kwenye mchezo huo miongoni mwa nyota ambao wanatoka KMC ni pamoja na mkongwe Juma Kaseja ambaye ni kipa namba moja naye alikuwa kwenye orodha ya wachezaji wa Stars ambao walishinda bao 1-0 dhidi ya Libya.
Pia wachezaji wa KMC walikuwa kwenye mapumziko ya siku nane kuanzia Machi 11 na walipaswa kurejea Machi 20 kutokana na msiba wa aliyekuwa Rais wa Tanzania awamu ya tano, John Pombe Magufuli uliotokea Machi 17 waliongezewa siku za kurejea kambini.
Jana Machi 28 wachezaji wameripoti kambini kwa ajili ya kuanza maandalizi ya mechi zao zijazo ndani ya msimu wa 2020/21.
KMC FC ipo katika nafasi ya tano kwenye msimamo wa ligi na ina alama 35 ambapo katika mchezo wake wa mwisho kabla ya kwenda kwenye mapumziko mafupi ilikutana na Ruvu Shooting Uwanja wa Uhuru Jijini Dar es Salaam na kuibuka na ushindi wa bao 1-0.