DIDIER Gomes, Kocha Mkuu wa Simba amesema kuwa kikubwa ambacho kinawapa nguvu ya kuamini kwamba watapata matokeo mbele ya AS Vita ni pamoja na hali ya kujiamini na maandalizi mazuri.
Kikosi cha Simba kinatarajiwa kumenyana na AS Vita kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika unaotarajiwa kuchezwa Aprili 3, Uwanja wa Mkapa.
Mfaransa huyo ameongeza kwamba kuchukulia siriazi na kujiamini katika mechi zao ndiyo kitu ambacho kimekuwa kikiwabeba na kuifanya timu hiyo kutopoteza mechi yoyote hadi sasa katika Ligi ya Mabingwa Afrika.
Simba ni vinara wa Kundi A la Ligi ya Mabingwa Afrika watakuwa uwanjani kupambana na Vita katika mechi ambayo Simba wakitoa sare tu watajihakikishia nafasi ya kwenda hatua ya robo fainali, lakini Vita wanahitaji ushindi tu ili wafufue matumaini yao ya kutinga robo fainali.
Gomes amesema kwamba kila mechi ambayo wamekuwa wakiicheza katika hatua hiyo wamekuwa wakiamini kwamba wanaweza kupata matokeo na hiyo imekuwa msaada mkubwa kwao.
“Mchezo wetu ujao dhidi ya AS Vita ni muhimu kwetu kushinda kwani tunahitaji pointi tatu ili kufikia malengo ambayo tumejiwekea.
“Tuko siriazi kwenye kila mechi ya hatua hii kwa ajili ya kuwa bora zaidi baadaye. Tunajiamini kwenye kila mechi kwamba tuna uwezo wa kufanya vizuri na mara zote imekuwa ikitokea hali hiyo.”
Gomes ameanza maandalizi na baadhi ya wachezaji wake ambao hawakuitwa kwenye timu zao za taifa katika viwanja vya Simba Mo Arena maeneo ya Bunju ikiwa ni pamoja na Bernard Morrison, Chris Mugalu, Ibrahim Ajibu, Miraj Athuman.