Home Simba SC GOMES :- SIMBA BADO SANA KWA UBINGWA WA AFRICA

GOMES :- SIMBA BADO SANA KWA UBINGWA WA AFRICA

 


IMETIMIA miezi miwili na nusu tangu kocha wa Simba, Didier Gomes Da Rosa apewe kazi ya kukinoa kikosi hicho baada ya kuachana na aliyekuwa kocha wao, Sven Vandenbroeck.

Simba ilimtangaza Gomes kuwa kocha mkuu, Januari 24, 2021 na siku hiyo hiyo jioni aliibuka kwenye mazoezi yanayofanyika kwenye Uwanja wa Mo Simba Arena uliopo Bunju nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam.

Mabosi wa Simba walifanya uamuzi huo baada ya Sven kuondoka katika wakati ambao hawakutarajia kwani siku moja nyuma alikuwa ametoka kuipa timu hiyo mafanikio kwa kuipeleka hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Gazeti la Mwanaspoti limefanya mahojiano maalumu na Gomes ambaye amefunguka mambo mengi tangu alipofika nchini mpaka wakati huu.

MTIHANI WAKE

Simba wamempa kocha huyo malengo matatu ambayo anatakiwa kuyafikia baada ya msimu kumalizika na kama ikishindikana huenda akaonyeshwa mlango wa kutokea.

Gomes anasema katika mkataba wake amewekewa lengo la kuhakikisha timu hiyo inacheza hatua ya nusu fainali Ligi ya Mabingwa Afrika ambapo sasa wapo hatua ya makundi.

“Kuifikisha timu kwenye hatua hiyo inawezekana kutokana na ushirikiano ambao naupata kutoka kwa viongozi, wasaidizi wangu pamoja na wachezaji wenye kiu ya mafanikio,” anasema.

“Ukiangalia tunaongoza msimamo wa kundi na tumebakiwa na michezo miwili – mmoja ambao tutacheza nyumbani dhidi ya AS Vita na mwingine wa mwisho ugenini dhidi ya Al Ahly, kama tukifanya vizuri ni wazi tunaweza kumaliza vinara wa kundi.

“Malengo mengine mawili natakiwa kutetea ubingwa wa Ligi Kuu Bara ambao mwenendo wetu sio mbaya pamoja na Kombe la Shirikisho (ASFC), ukiangalia katika mashindano yote hayo mwenendo wetu si mbaya na tunaweza kuyafanikisha hayo yote.”

MIPANGO YAKE

Gomes anasema ili aweze kufikia malengo aliyowekewa na mabosi wake ni lazima awe na mipango ambayo itamfikisha mwisho wa msimu akifurahi.

Anasema amepanga kukitengeneza kikosi chake kuwa bora na tishio sio katika mashindano ya ndani, bali hata ya kimataifa ambayo wamekuwa na malengo ya kufanikiwa muda mrefu.

“Baada ya kuitengeneza Simba kuwa tishio kwa muda wote ambao nitakuwa hapa nataka iwe timu yenye mazoea ya kuchukua makombe mbalimbali katika kila shindano ambalo litakuwepo au kuanzishwa.

“Nilipata nafasi ya kuona timu ya vijana (ya Simba), lakini sikubahatika kukaa nao, ila kuna mipango na mifumo ambayo nitaiweka huko ili kufanikiwa kupata wachezaji ambao watakuwa bora, inawezekana wasicheze Simba kwa wakati huu, ila siku za mbeleni.

“Ni mipango mikubwa ambayo ninayo na ndio maana nafanya yote haya kuhakikisha timu inafikia yale malengo ambayo tumejiwekea mwanzo wa msimu,” anasema Gomes aliyezaliwa Oktoba 1, 1969

UBINGWA AFRIKA

Miongoni mwa malengo ya muda mrefu ambayo viongozi wa Simba wamekuwa wakiyaeleza ni kutwaa ubingwa wa Afrika kwa miaka ijayo.

Gomes anasema analifahamu hilo na hata wakati anaajiriwa Simba miongoni mwa mambo aliyoambiwa ni la kutwaa ubingwa wa Afrika likiwa katika malengo ya muda mrefu.

“Kwa ambavyo nimeiona Simba wakati huu haitaweza kutwaa ubingwa wa Afrika, ila inaweza kucheza nusu fainali kama tutacheza vizuri michezo yetu,” anasema.

“Lakini kama kutakuwa na mwendelezo wa namna hii katika kuendesha timu, kufanya usajili na mambo mengi ya msingi ndani ya miaka mitano ijayo Simba inaweza kuwa miongoni mwa timu ambazo zinaweza kutwaa ubingwa wa Afrika.

“Ukiangalia ambavyo Simba wanaishi na viongozi wao wanashirikiana katika utendaji wa kazi kama baadhi ya timu kubwa Afrika, ila wanakosa uzoefu wa kufika hatua kubwa ya robo au nusu fainali.

“Kama wakifanikiwa kufanya hivyo ndani ya misimu miwili mfululizo wanaweza kucheza fainali na wakatwaa ubingwa wa Afrika jambo ambalo sio rahisi, lakini kwa maendeleo na mwenendo hilo linawezekana.”

NGUVU YA UONGOZI

Viongozi wa Simba wamegawanyika maeneo mbalimbali kwenye utendaji wa kazi. Kuna wanaosimamia mashindano ya ndani, wapo wanaoungana na timu mahala popote ambapo inasafiri, wapo wanaosimamia usajili pamoja na maeneo mengine.

Gomes anasema amekuwa anafurahishwa na nguvu hiyo ya viongozi.

“Silaha ya kwanza ya Simba ni maelewano na usikivu wa viongozi ambao wamekuwa wakifanya kazi kwa kushirikiana na manufaa yao huwa yanachangia mafanikio ya timu.

“Kama nikikutana na changamoto ambayo nahitaji ifanyiwe kazi napata majibu kwa haraka. Timu ikisafiri mahala popote wanakuwepo, kama kuna jambo ambalo nataka lifanyiwe kazi kwa haraka linakuwa hivyo.

“Natambua mchango wao na kama wakiendelea hivi sioni sababu ya Simba kushindwa kufanya vizuri kwenye mashindano ya kimataifa pamoja na mengine ya ndani,” anasema Gomes.

SOMA NA HII  KIUNGO HOROYA AINGIWA NA HOFU..."NI NGUMU KUSHINDA MECHI HII....TUTAJARIBU KUPATA USHINDI

KIKOSI BORA

Gomes anasema amefundisha timu nyingi mpaka wakati huu, ila kwenye kikosi cha Simba amekutana na wachezaji wengi ambao wana viwango bora mpaka wengine wanashindwa kucheza mara kwa mara.

“Katika baadhi ya timu ambazo nimewahi kufundisha ukiwatoa wachezaji 11 ambao wanaanza kikosi cha kwanza wengine waliobaki ni bora kama ambao wapo uwanjani.

“Simba mambo yamekuwa tofauti, wale wachezaji 11 ambao wapo kikosi cha kwanza wengine waliokuwa benchi la akiba na wale ambao wapo jukwaani wanaweza kucheza kama waliopo uwanjani.

“Nimevutiwa na kikosi hiki, kina wachezaji bora kulingana na majukumu ya nafasi ambazo wanazitumikia na nikiangalia timu ilivyo bora kwa mashindano ya hapa ndani tutaendelea kuwa chaguo la kwanza,” anasema.

BENCHI LA UFUNDI

Gomes alianza kazi bila kuwa na msaidizi mwingine kama walivyo baadhi ya makocha wanapopata kazi mpya wanakwenda na wasaidizi wao.

“Tangu nimeanza kazi kwenye timu hii nimekuwa nikifanya vizuri majukumu yangu kwa kushirikiana na wasaidizi wangu katika benchi na kila mmoja amekuwa akifanya kazi yake kwa ushirikiano na weledi mkubwa.

“Mpaka Simba inafanikiwa kufanya vizuri, basi ujue kila mmoja ambaye yupo kwenye benchi ametimiza majukumu yake ya kazi kama ipasavyo mpaka tunafikia malengo yetu.

“Kimsingi nimekuwa nikipata ushirikiano na kufurahishwa na utendaji kazi wa wasaidizi wangu wote ambao nimewakuta hapa,” anasema Gomes ambaye aliwahi kuchukua ubingwa wa Ligi Kuu Rwanda msimu wa 2013 akiwa na Rayon.

NGUVU YA MASHABIKI

Simba katika mechi zake za ligi mahala popote ambapo inakwenda kucheza hukutana na shangwe la kutosha kutoka kwa mashabiki wao bila ya kujali wako uwanja gani.

Gomes anasema soka la Tanzania litakuwa na maendeleo kutokana na mashabiki wa soka nchini kupenda timu zao na kuzishangilia katika viwanja mbalimbali ambavyo hucheza.

“Binafsi nitambue nguvu ya mashabiki wa Simba, kiukweli mchango wao ni mkubwa, wanapokuwa uwanjani hutushangilia na kutopa morali kuanzia benchi mpaka wachezaji kupambana zaidi ya awali.

“Unajua mchezo wa soka unahusisha hisia, kama unakuta kuna watu wamejaa majukwaani wanatamani ufanye jambo fulani pengine hata kama huna uwezo huo unajikuta umelifanya ili kuhakikisha unawapa furaha,” anasema Gomes.

USHINDANI BARA

Simba inashika nafasi ya pili kwenye msimamo wa Ligi Kuu Bara na kama ikishinda mechi za viporo inaweza kuwa kinara wa ligi ambayo sasa inaongozwa na Yanga.

Gomes anasema miongoni mwa ligi ambazo amewahi kufundisha na kukutana na ushindani ni ya Bongo kwani kila timu inatamani kufanya vizuri. “Ushindani umekuwa mkubwa mno, ukiangalia kila timu ambayo inakutana na Simba lazima inatamani kufanya vizuri jambo ambalo unatakiwa kuandaa mbinu za maana kuwapatia wachezaji ili wafanye vizuri.

“Ukiangalia aina ya ushindani ambao tunakutana nao kama ule tulioupata dhidi ya Prisons ni ishara tosha kuwa msimu huu ligi ni ngumu na tunatakiwa kufanya kazi ya ziada ili kufikia malengo ya kutwaa ubingwa,” anasema.

MBINU ZAKE

Gomes anasema mara nyingi kikosi chake hupenda kucheza soka na kushambulia zaidi wanapokuwa uwanja wa nyumbani, lakini ugenini hubadilisha mbinu zake. “Unajua unapokuwa nyumbani unakuwa na kiu ya kupata alama tatu kutokana na mazingira mengi mazuri yanayokuwa upande wako, lakini ugenini unatakiwa kuwa na nidhamu kubwa,” anasema.

“Ukiangalia katika mashindano haya ya kimataifa muda mwingi tunakuwa na nidhamu katika kuzuia mashambulizi ya timu pinzani na kufanya mashambulizi ya kushtukiza ambayo hutusaidia kufanya vizuri kama ilivyokuwa mechi na AS Vita.

“Mechi zetu za nyumbani ukiangalia muda mwingi tunashambulia zaidi ya vile ambavyo tunafanya ugenini, lakini tunakuwa na tahadhari ya wapinzani katika kucheza kwao na ni hivyo huwa tunafanya katika mechi za ligi.”

NAMBA USHINDANI

Simba ina wachezaji 30 na katika kila mechi wanatakiwa kuvaa jezi wachezaji 18 ambapo 11 wataanza na saba kuwa benchi la akiba huku 12 wanabaki jukwaani.

Gomes anasema katika orodha ya wachezaji wake wote ni bora, lakini huwatumia kulingana na mahitaji ya mechi ilivyo, ila kuna wengine anawaweka benchi sio kwa kuwa viwango ni vidogo. “Ukubwa wa Simba unaanzia hapa kwa wachezaji nilionao, kuna muda mpaka kichwa kinauma kwani wote wanafanya vizuri mazoezini na wanastahili kupewa nafasi ya kucheza ila nalazimika kuwaweka benchi kutokana na idadi ambayo inahitajika

“Nadhani unaona ushindani wa namba kwenye mazoezi yetu, kila mchezaji anastahili kupewa nafasi ya kucheza lakini inakuwa haina jinsi lazima utamuweka nje kulingana na idadi ambayo inahitajika ila sio suala la kiwango,” anasema kocha huyo.