Home Simba SC MAKALA | MUGALU NA FUMBO LA MSHAMBULIAJI NAMBA TISA WA KISASA

MAKALA | MUGALU NA FUMBO LA MSHAMBULIAJI NAMBA TISA WA KISASA

ZIKO nchi au timu duniani ambako jezi namba tisa ni nzito kuvaliwa.

Uzito wa jezi haupimwi kwa kilo au ujazo. Uzito wa jezi hupimwa kutokana na historia ya watu waliotangulia kuivaa au klabu yenyewe husika.

Namkumbuka sana mchezaji mmoja mpya kijana wa kitanzania aliyesajiliwa kwa mbwembwe kujiunga na timu ya samba lakini baada ya mazoezi ya wiki moja tu mtu mmoja akaja kuniambia kwamba huyo mchezaji hatacheza kwa sababu jezi imemzidi.

Miezi mitatu baadaye, mchezaji alikuja kwangu; wakati huo nikiwa kiongozi wa samba na kuniomba nimruhusu arudi katika klabu aliyotoka.

Yeye alikuwa na maelezo yake tofauti kabisa lakini nilikumbuka maneno ya yule mzee kwamba kwa kijana yule, tatizo lake kubwa zaidi lilikuwa uzito wa jezi.

Wachezaji huvaa jezi tofauti uwanjani kwa ajili ya kuwatofautisha. Mazoea katika vilabu vingi ni kwamba kuna jezi walau tatu ambazo mara nyingi huwa na maana kubwa kwa washabiki. Jezi hizo ni namba 10, 7 na 9.

Wako nyota waliowahi kuvaa jezi namba nyingine; kuanzia makipa na mabeki kama kina Paolo Maldini, lakini namba hizo tatu zina maana kubwa katika klabu kingine.

Jezi hizo huwa na watu walioacha kumbukumbu nyingi kwa ama kupachika mabao au kutengeneza nafasi nyingi kwa wengine kufunga.

Huko zamani, jezi namba tisa ilimaanisha mfungaji. Kila mchezaji, katika mazingira ya kawaida, anaweza kufunga kwa sababu kazi hiyo kwa mujibu wa Bill Shankly, ni sawa tu na kupasia mpira kwenye wavu wa adui.

Hata hivyo, hawa namba tisa wa kizamani ni watu tofauti kidogo. Walikuwa wanajua goli lilipo, wabinafsi, wana roho ngumu na hawakati tamaa. Wakati mwingine hata kumiliki mpira tu kwao ilikuwa tatizo.

Ndio sababu, nyota wa zamani wa Arsenal na Ufaransa, Thierry Henry, aligoma kabisa kuitwa mfungaji. Alisema yeye ni mshambuliaji na kwa makusudi kabisa akawa hakai kwenye boksi. Akawa anapenda kutokea pembeni, kukimbia kidogo machejo ya hapa na pale na halafu anafunga. Hakutaka kuwekwa kapu moja na kina Gerd Muller, Gabriel Batistuta, Filipo Inzaghi, Mohammed Hussein ‘Mmachinga’ na Emmanuel Gabriel.

Henry na wenzake ndio wamebadili aina ya washambuliaji tulionao sasa. Timu nyingi sasa zinatumia namba tisa ambao si lazima wafunge sana, lakini wanasaidia sana timu zao kucheza kwa aina tofauti. Anaweza asifunge sana lakini timu inaweza kufunga zaidi akiwepo.

SOMA NA HII  WAKATI SIMBA WAKITAKA KUACHANA NAYE....HIVI NDIVYO KLABU ZA CONGO NA ZAMBIA ZINAVYOMPAPATIKIA CHRISS MUGALU...

Nakumbuka sana mazungumzo niliyowahi kufanya na aliyewahi kuwa nyota wa Simba, Emmanuel Okwi, takribani miaka nane iliyopita.

Siku hiyo Okwi alikuwa amerudi Dar es Salaam kutoka kwao Uganda alikokuwa ameenda kwa ruhusa maalumu. Alipokuja mazoezini, alikuta Simba ina mshambuliaji mpya aliyeitwa Felix Sunzu.

Wakati mazoezi yakiendelea, Okwi alishindwa kuvumilia. Alinifuata na kuniambia, “Kiongozi, unaona, yule sasa ndio namba tisa wa kisasa.”

Okwi alikuwa ameona kitu ambacho mwenzake huyo alikuwa anafanya. Katika muda waliocheza pamoja na kuwapa Wekundu wa Msimbazi mafanikio, Sunzu na Okwi walikuwa kama unavyoona Karim Benzema na Cristiano Ronaldo au ilivyo kwa kina Mohamed Salah na Bobby Firmino.

Sunzu alikuwa mpachika mabao pia lakini uwezo wake wa kucheza mipira ya juu, kukaba na kukaa na mpira ulikuwa msaada mkubwa kwa okwi aliyekuwa akishambulia kutokea pembeni kama ilivyokuwa kwa kina Henry.

Ndio jambo ambalo sasa naliona kwa mshambuliaji mpya wa Simba, Chris Kope Mugalu. Hakuna mechi ambayo nadhani nilimwelewa zaidi kuliko ile dhidi ya AS Vita iliyochezwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Alifunga bao moja kwa njia ya penalti, lakini uwezo wake wa kukaa na mpira na kusaidia timu kusogea mbele ndiyo ulionikosha zaidi.

Nimemtazama tena katika mechi dhidi ya Tanzania Prisons wiki hii kwenye Ligi Kuu Bara na nimejiridhisha kwamba Mugalu ni namba tisa wa kisasa.

Kama angekuwa dizaini ya kina Gabriel, angeweza kuweka wavuni hata mabao matatu. Alipata nafasi za kutosha kufunga mabao hayo lakini alisaidia timu kwa namna ya kisasa ya namba tisa wa leo.

Kama marehemu Adam Sabu akifufuka leo kutoka kuzimu na akatazama mechi ya Simba, atajiuliza maswali yote kuhusu Chris Mugalu kwamba ana sifa zote za kimwili za namba tisa wa zamani lakini idadi ya mabao anayofunga ni ndogo.

Lakini, akiwa katika mawazo, nina uhakika Abdallah Kibadeni atampigapiga makofi mgongoni na kumwambia neno moja kazi hiyo ya kufunga mwenyewe ni John Bocco ‘Adebayor’.