Home Yanga SC MWAMBUSI AFUNGUKA A-Z SABABU ZA KUONDOKA YANGA NA KURUDI

MWAMBUSI AFUNGUKA A-Z SABABU ZA KUONDOKA YANGA NA KURUDI


KAIMU Kocha Mkuu wa Yanga, Juma Mwambusi amekaa na staa wa timu hiyo,Carlos Carlinhos kutoka Angola na kumpa uhalisia wa kile ambacho klabu na mashabiki wanakitaka kutoka kwake na anapaswa kukifanya kwa haraka kadri inavyowezekana kulinda thamani yake.

Mwambusi ambaye ni muumini mkubwa wa nidhamu tangu akiwa Mbeya City na Prisons, alisema mchezaji huyo ni kati ya mastaa ambao wanapaswa kufanya kazi kubwa kutetea heshima yao na klabu kuanzia sasa Yanga inaposaka ubingwa kwa nguvu zote.

Carlinhos alijiunga na Yanga Agosti mwaka jana akitokea Interclube ya kwao, Angola, ingawa bado hajawa na msimu mzuri kwenye kikosi hicho kilichomtimua Kocha Cedrick Kaze wa Burundi na sasa kinakamilisha kumshusha nchini dakika yoyote Kocha Mfaransa, Sebastian Migne.

“Yanga tuna mapro(wachezaji wa kimataifa) wengi, hivyo kuwaunganisha kuwa kitu kimoja si kazi nyepesi, ila nimeianza na inakwenda vizuri. Nafahamu watu wamekuwa wakijiuliza kuhusu Carlinhos, niliporudi Yanga nimefanya nae mazoezi kabla hajaondoka kurudi kwao,”anasema Mwambusi.

Anasema mchezaji huyo ana kipaji cha mpira, japo sasa ana matatizo ya kifamilia mkewe wake kajifungua, hivyo ameomba kwenda kwao.

“Kabla hajaondoka nilizungumza naye ni mchezaji mwenye kipaji cha hali ya juu sana kwenye soka, ila anapaswa kurudisha thamani yake, aonyeshe kile ambacho Wanayanga wanakitamani kukiona kutoka kwake kisoka.

“Aisaidie timu, hicho ndicho cha muhimu kwake hivi sasa na akifanya hivyo, watu wataelewa kwanini nasema ni mchezaji mwenye kipaji,”aliongeza Mwambusi ambaye Mwanaspoti linajua kwamba bosi wake, Migne tayari ameshaanza kupitia faili moja baada ya lingine ya wachezaji waliopo kikosini baada ya kumalizana na uongozi. 

Habari za uhakika ambazo gazeti la Mwanaspoti imezipata kutoka ndani ya Yanga ni kwamba Kocha huyo amepania kufanya mabadiliko makubwa kikosini na amewaambia atahitaji wiki tatu tu kuelewa kiundani kila staa ingawa ameahidi kumuachia Mwambusi sehemu kubwa ya kumalizia msimu.

TATIZO LA MASTAA

Mwambusi ambaye anasifika kwa mazoezi ya fiziki anasema alipotua Yanga alibaini wachezaji wake wanahitaji kujengwa kisaikolojia.

“Kulikuwa na changamoto ya mashabiki kutofurahia matokeo ya timu, niliwambia ni kweli mashabiki wanaumizwa na matokeo na ni haki yao, lakini je? suluhisho ni nini?,” anasema Mwambusi ambaye timu yake inaongoza msimamo wa Ligi ikiwa na pointi 50 na haijapoteza msimu huu.

“Nilianza na saikolojia, niliwaeleza wakati wa changamoto, timu inakuwa hivi na vile,hivyo hata kwao ni wakati wa mpito.

“Niliwaeleza uwezo wao na hali ilivyo huko kwa mashabiki, japo niliwataka wasiingize kile kinachofanyika nje katika akili zao, wao wacheze mpira.

“Niliwaeleza pia wanapaswa kuwaheshimu mashabiki, wanachama na wapenzi kwa kuwa wana uchungu pale timu yao inapofanya vibaya, lakini ili kuwatuliza, lazima tupambane tushinde,”alisema Kocha huyo wa zamani wa Azam.

“Nilibaini kuna changamoto ndogo ndogo, tulizungumza na kila mmoja alikubali kujitoa kwa ajili ya timu, tuliamua kutochanganywa na maneno ya nje na ili tuyatulize lazima tushinde tu hakuna njia nyingine,”anasema na kuongeza kingine alichohitaji kifanyike kwenye timu hiyo ni nidhamu kwa wachezaji wote.

“Kwenye nidhamu,kocha lazima uwe mfano na wao wajifunze kupitia wewe na warudishe kile unachokitaka wafanye,”anasema Kocha huyo ambae mtihani wake wa kwanza ni dhidi ya Prisons kwenye Kombe la FA.

Mwambusi anasema yeye muumini wa nidhamu, anapenda wachezaji wanaofundishwa naye wapite kwenye mkondo huo.

“Nimeihamishia falsafa hiyo Yanga kwa kuwa niko huko na bahati nzuri nimerudi Yanga na kuikuta timu ikiwa na msukumo wa mafanikio, wachezaji walikuwa wana shauku ya kufanya vizuri, hivyo sikupata taabu,”anasema na kuongeza kuwa alianza kwa kuwakumbushana majukumu ya kila mmoja ndani ya timu na wachezaji wameahidi kufanya vizuri na kuiendeleza Yanga iinuke zaidi kisoka.

WALIOMALIZA MIKATABA

Mwishoni mwa msimu nyota kadhaa akiwamo kipa Metacha Mnata na Said Juma Makapu watamaliza mikataba yao ambayo kocha Mwambusi anaeleza hatma ya nyota hao.

“Mwishoni mwa msimu tutaangalia, kuna wachezaji ambao watauzwa, wapo wanaomaliza mkataba na wapo ambao klabu itaamua kuachana nao hivyo tuwe na subira .

“Ndiyo nimeanza kupitia mkataba wa mmoja mmoja kwenye timu, hivyo tuwe na subira na uongozi italitolea tamko mwishoni mwa msimu,”anasema.

SOMA NA HII  WACHEZAJI WA YANGA WAMVURUGA GAMONDI AFANYA MAAMUZI MAGUMU

SIRI ZA PLUIJM, ZLATKO

Katika maisha yake ya ukocha, Mwambusi amewataja makocha watatu wa kigeni ambao alifanya nao kazi vema.

“Hans Pluijm ndiye kocha niliyefanya naye kazi vizuri zaidi kwenye maisha yangu ya soka. Japo Lwandamina (George raia wa Zambia) Zlatko(Serbia) pia nimefanya nao kazi vizuri sana, katika historia yangu ya soka, hawa ndiyo makocha wa kigeni ambao siwezi kuwasahau,” anasema.

KUPANGIWA TIMU

“Kwangu kila mtu yuko huru kushauri, ila naangalia nimestiki wapi katika kuifanikisha timu na si kuingiliwa kwenye majukumu,”anasema.

Hata hivyo Mwambusi amebainisha kwamba hajawahi kukutana na changamoto ya uongozi kuingilia majukumu yake kama kocha, si tu Yanga bali katika timu zote alizowahi kufundisha.

KWANINI ALIONDOKA?

“Awali mkataba wangu ulikwisha nikaondoka, wakanirejesha lakini nilipoondoka mara ya mwisho niliomba mwenyewe.”

“Nilisumbuliwa na mshipa mmoja unaotoka kichwani unapita kwenye jino hivyo daktari alinishauri nipumzike, sikuwa nimemaliza mkataba na Yanga, hata hivyo waliniruhusu.

“Nilitibiwa na kupona, lakini wakati huo tayari Yanga ilikuwa na benchi la ufundi jingine, hivyo nikawa naendelea na maisha mengine,” anasema wala hakuwa na tofauti Kaze wala kocha yoyote aliyepita.

“Nilikuwa nimepona wakati huo na ikumbukwe nilipo ondoka Yanga nilikuwa bado na mkataba, waliniruhusu kwenda kwenye matibabu, hivyo waliponieleza kuhusu kurudi ilikuwa narudi kuendelea kuutumikia mkataba wangu wa awali,” anasema.

NDOTO NNE

Mwambusi ambaye aliingia kwenye ukocha baada ya baba yake mzazi kumkataza asicheze mpira anasema katika maisha yake ya ukocha ana ndoto nne.

“Unajua nilijifunza soka kwa kucheza utotoni baada ya kuangalia namna watu wanavyoc heza hadi nikawa mchezaji mzuri, bahati mbaya familia yangu hasa baba hakupenda kabisa niwe mwanasoka,” anasema mzee wake alikuwa anaogopa asipate majeraha.

“Nilimsikiliza ila nikamuomba niingie kwenye ukocha kwa kuwa soka ilikuwa kwenye damu, alinikubalia ndipo nikaanza kusoma ukocha hadi sasa.

“Nikiwa huko niliapa kwamba lazima nitimize ndoto nne, kwanza ni kuchukua ubingwa, pili ni kuvaa medali, tatu ni kufundisha timu kubwa na mwisho ni kuifundisha Taifa Stars.

“Naamini ndoto tatu zimetimia na nitaendelea kuziishi mara kwa mara, bado moja ya kuifundisha Stars, ila pia naamini itatimia na utafika wakati viogozi wataona Mwambusi anatufaa na watanipa mkataba,” anasema.

KUMBE ALILIA

Mwambusi akiwa kocha wa Moro United alilia. “Tulikuwa na mechi na namna nilivyokiandaa kikosi changu niliamini tunashinda, nilipanga timu na kila mmoja nikampa majukumu yake.

“Niliwambia wachezaji katika hiyo mechi kuna dalili tutapata penati, hivyo ikitokea tukapata itapigwa na Stephano Mwasyika,”.

Anasema kwenye timu yake wakati ule wapigaji wazuri wa penati alikuwa ni Yona Ndambila, Mwasyika na Nasoro Masoud ‘Chollo’.

“Kweli dakika ya saba ya mchezo tukapata penati, ikatokea mchezaji ambaye sikumpanga apige ndiye amewahi kwenda kuipiga, nilinyanyuka nikawa namuita aache jukumu hilo kwa mtu niliyempanga.

“Kwenye benchi wakasema kocha muache tu kwa kuwa ameshakwenda kupiga, ukimtoa itakuwa siyo, wewe muache tu, lakini sikutaka kabisa Hussein Swedi apige ile penati na sikumpanga.”

“Niliumia mno siku hiyo sitokaa nisahau, halafu tukafungwa mabao 2-1, yaani ni tukio ambalo katika maisha yangu ya soka liliniumiza.”

MAFANIKIO MBEYA CITY

Akiwa kocha wa Mbeya City,ilimaliza kwenye nafasi tatu za juu kwenye Ligi baada ya kupanda daraja mwaka 2013 ikiwa timu changa kwenye Ligi Kuu Tanzania Bara.

“Hiyo ilitokana na kujitoa kwa wachezaji, uongozi, wanachama na mashabiki wetu, kila mmoja alitimiza wajibu wake na timu ilijengwa katika misingi ya nidhamu ya hali ya juu ndiyo sababu tulifanikiwa.

“Muundo huo sasa nataka uwe Yanga, nidhamu, kujitoa kwa wachezaji na hata ushirikiano, mazoezi ndivyo viwe nguzo kwetu, naamini tutafanya vizuri na ubingwa utakuwa wetu tu,”.

“Ligi bado mbichi kabisa, mechi 10 au 13 si mechi ndogo, wacha muda ufike, wakati muafaka wa ubingwa bado, tunaangalia mechi ijayo, ushindi katika mechi zetu ndiyo utatupa mwanga wa ubingwa ambao tunaamini msimu huu ni wetu,”.