Home Yanga SC LUC EYMAEL ‘AWARUDI’ YANGA KIVINGINE

LUC EYMAEL ‘AWARUDI’ YANGA KIVINGINE


Kocha wa zamani wa Yanga, Luc Eymael amesema kama timu hiyo inataka kufanikiwa na kutisha katika Ligi Kuu Bara pamoja na michuano ya kimataifa inapaswa kuvumilia na kujenga timu ya ushindani.

Eymael ameeleza kuwa hakuna njia ya mkato kwa timu ya soka kufikia mafanikio iwapo itakuwa haina uvumilivu kwa makocha.

Kocha huyo ambaye kwa sasa yupo nchini Ubelgiji, alisema Simba ndiyo klabu bora Afrika Mashariki kutokana na inachokifanya katika Ligi ya Mabingwa Afrika na hilo linapaswa kuwa somo kwa Yanga kuacha timuatimua ya makocha kwa sababu haiwezi kufika mbali.

Eymael alisema ni vyema viongozi wakatambua kujenga timu siyo suala la siku chache na haiwezekani kila msimu kuwa na usajili wa idadi kubwa ya wachezaji kisha itegemee ndani ya msimu huo kutwaa ubingwa.

“Siku zote makocha huwa roho juu kwa sababu kazi zetu hazina dhamana, muda wowote unaweza kufukuzwa. Nilisikia kuwa walimfukuza Kaze (Cedric) baada ya miezi mitano nikajiuliza nini kilikuwa kibaya mbona huu ni msimu wake wa kwanza na bado timu ipo kileleni? Sikupenda hilo kulipa nafasi kichwani,” alisema kocha huyo aliyetimuliwa Jangwani kwa matamshi ya kibaguzi aliyoyatoa.

Eymael aliongeza kuwa kocha mpya atakayetua Yanga anaweza asiwe na maisha marefu kama asipopewa muda wa kuijenga. Kocha huyo aliiongoza Yanga kumaliza msimu wa 2019/20 katika nafasi ya pili nyuma ya Simba.

SOMA NA HII  KISA OKRAH....MASTAA HAWA 'KUPIGWA PANGA' YANGA....ISHU NZIMA HII HAPA...