UJUMBE wa Kocha Mkuu wa Al Ahly ya Misri aliompa Ofisa Habari wa Simba umetimia kwa vitendo baada ya wawakilishi hao wa Tanzania katika Ligi ya Mabingwa Afrika kukubali kichapo cha bao 1-0.
Mchezo huo uliochezwa Uwanja wa Al Salam ulikuwa ni wa kisasi kwa Waarabu hao wa Misri kwa sababu mchezo wa kwanza walipocheza na Simba, Uwanja wa Mkapa walikubali kufungwa bao 1-0 lililofungwa na Luis Miquissone.
Jana, kabla ya mchezo, Pitso Mosimane ambaye ni Kocha Mkuu wa Al Ahly, alimwambia Haji Manara kuwa watawafunga kwenye mchezo huo jambo ambalo lilitimia dakika 90 zilipokamilika.
Manara alisema kuwa walipokutana na Mosimane kabla ya mchezo wa jana, kocha huyo alimwambia kwamba Klabu ya Simba ni imara ikiwa Uwanja wa Mkapa ila inapotoka nje haina ubora.
Maneno hayo yalimchoma Manara ambaye anasema kuwa aliamua kumwambia pia kocha wa timu ya Simba, Didier Gomes na kubeba matumaini kwamba wangeweza kuonesha namna ambavyo Simba inafanana.
Bao la ushindi kwa Al Ahly lilipachikwa na Mohamed Sherif dakika ya 31 na kuifanya Simba kubaki na pointi zake 13 ikiwa ni kinara wa kundi A huku Al Ahly ikiwa nafasi ya pili na pointi 11.