AMRI Said aliyekuwa kocha mkuu wa Klabu ya Mwadui FC amesema kuwa sababu iliyomfanya abwage manyanga ni kushindwa kulipwa stahiki zake kwa wakati.
Said ambaye alifutwa kazi ndani ya kikosi cha Mbeya City kutokana na timu hiyo kuwa na mwendo mbovu alipewa kazi ya kukinoa kikosi cha Mwadui FC baada ya uongozi wa timu hiyo kumfuta kazi Khalid Adam.
Khalid naye alifutwa Mwadui FC kutokana na mwendo mbovu wa timu hiyo ambayo ipo nafasi ya 18 kwenye msimamo mechi yake ya mwisho kukaa benchi alishuhudia timu yake ikikubali kichapo cha mabao 5-0 dhidi ya Yanga.
Said amesema:”Nilikuwa naona kwamba sijalipwa stahiki zangu na hakuna ambacho nilikuwa ninaambiwa jambo ambalo limenifanya niamue kujiweka kando,”.
Kocha huyo mwenye uzoefu na soka la Bongo aliwahi kuifundisha Klabu ya Mbao FC, Biashara United na pia alikuwa kwenye hesabu za kutua Ndanda FC ila dili lake lilibuma kabla hajapewa mikoba ya Malale Hamsini ambaye kwa sasa yupo Polisi Tanzania.