BEKI kisiki wa Simba chaguo namba moja la Kocha Mkuu, Didier Gomes, Joash Onyango amesema kuwa wanaomba wafike hatua ya nusu fainali kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika.
Simba imefanikiwa kutinga hatua ya robo fainali baada ya kukusanya pointi 13 kwenye kundi A ikiwa ni namba moja huku Al Ahly wakiwa nafasi ya pili baada ya kukusanya pointi 11.
Kwenye hatua ya makundi Simba ilicheza jumla ya mechi sita ambapo ilifungwa mechi moja ilikuwa mbele ya Al Ahly kwa kukubali kuokota bao moja nyavuni huku mechi nne ilishinda na ililazimisha sare ya bila kufungana na Al Merrikh ya Sudan.
Onyango amesema kuwa hatua ambayo wamefika ni kubwa na wanaamini wana nafasi ya kufanya vizuri kwenye hatua hiyo.
“Tunashukuru kufika hatua ya robo fainali licha ya kwamba tulipoteza mchezo wetu wa mwisho. Ila kwa sasa ambacho tunaomba ni kwamba tuweze kufika hatua ya nusu fainali kwani haya ni malengo yetu.
“Ushindani ni mkubwa hilo lipo wazi nasi pia hatutafanya vibaya tutapambana na kusaka matokeo kwenye mechi zetu,” amesema.