BAADA ya Jumanne ya Aprili 20, wiki hii Yanga kushusha makocha wawili wapya kwa ajili ya kuinoa timu hiyo, ikumbukwe kuwa Alhamisi ya Aprili 22 pia ilimshusha kocha mpya wa viungo, Jawadi Sabri ambaye baada ya kutua nchini aliahidi neema kibao kwa klabu hiyo.
Sabri mwenye uraia wa Morocco ana masters ya fitness ametua Yanga kuchukuwa nafasi ya Mghana, Edem Mortotsi aliyedumu kwa kipindi cha muda wa mwaka mmoja kama kocha wa viungo wa timu hiyo.
Tayari kocha huyo ameanza kazi Kigamboni akiwa na Kocha Mkuu, Nasreddine Nabi ambaye leo ana kibarua cha kuingoza timu hiyo kwenye mchezo wa ligi dhidi ya Azam FC, Uwanja wa Mkapa.
Kocha huyo amesema kuwa kuwa sehemu ya kikosi cha Yanga ni furaha kwake atatumia uzoefu wake kufanya kazi kwa vitendo na kushirikiana na wengine.
“Nafuraha kuona nakuwa sehemu ya kikosi cha Yanga kwani ni moja kati ya timu kubwa barani Afrika yenye mashabiki wengi wanaohitaji mafanikio makubwa katika mpira wa miguu. Mimi na wenzangu naamini tutashirikiana kuhakikisha tunakamilisha hilo, ” alisema kocha huyo.