Home Simba SC MWENDO WA MANULA, UNAZUNGUMZA KWA SAUTI YA JUU SANA

MWENDO WA MANULA, UNAZUNGUMZA KWA SAUTI YA JUU SANA


Na Saleh Ally

UKINIAMBIA hujasikia nitajua unafanya makusudi lakini kama utasema haujaelewa basi ninaweza kushirikiana na wewe tukajadili suala hili kwa ajili ya kujifunza.


Kwamba ukizungumzia wachezaji ambao wamekuwa gumzo katika suala la biashara, mmoja wapo ni kipa namba moja wa Simba na timu ya taifa, Taifa Stars.


Aishi Manula kwa sasa ni gumzo barani Afrika, anazungumzwa hadi katika ukanda wa Afrika Kaskazini na Afrika Kusini. Sehemu hizi mbili zinaongoza kwa mafanikio kisoka katika bara letu.


Sasa hawana ujanja, wanalazimika kumzungumzia Manula kutokana na namna kiwango chake kimekuwa juu na amekuwa na mchango mkubwa katika kikosi cha Simba.


Simba imecheza mechi sita za hatua za makundi, imefungwa mabao mawili tu. Pia imepoteza mchezo mmoja tu, mchezo ambao ilifungwa bao 1-0 ikiwa tayari imefuzu na kuwa kinara wa Kundi A huku vigogo na mabingwa watetezi, Al Ahly wakiwa katika nafasi ya pili.


Manula ambaye mwaka 2018, alikuwa mmoja wa makipa waliofungwa mabao mengi zaidi, mfano mechi tatu za ugenini alifungwa mabao 13, sasa amekuwa shujaa wa Simba na gumzo Afrika.


Huenda ingekuwa vigumu sana kusema na ikakubalika kwamba Manula ni kipa bora Tanzania kwa kipindi hiki kama Simba isingekuwa inashiriki michuano ya kimataifa.


Ilikuwa rahisi watani wao nao kusema Metacha Mnata ni zaidi ya Manula au vinginevyo, ingekuwa rahisi kusema kipa huyo anabebwa tu na difensi yake au vinginevyo. 

Lakini kazi kubwa aliyoifanya hasa katika hatua ya

makundi imekuwa mchango mkubwa kwa Simba kutinga robo fainali ikiwa na sura nyingine kabisa.


Mwenye macho haambiwi tazama, mwenye macho halazimishwi kukiangalia kinachotokea.

Ukweli uko wazi na tumeona katika mechi ngapi amekuwa shujaa wa Simba. Kawaida iko hivi, hakuna timu inayofikia mafanikio makubwa katika hatua za juu za Ligi ya Mabingwa Afrika bila ya kuwa na kipa bora.

Kipa anakuwa chachu kubwa ya safari na kikosi kufanya vizuri.


Manula amekuwa bora na msaada mkubwa, amekuwa akifuta kila kosa la safu yake ya ulinzi na wakati mwingine kuwa shujaa anayesababisha kupatikana kwa pointi tatu muhimu.

SOMA NA HII  KRAMO TIA MAJI TIA MAJI MAPYA YAIBUKA SIMBA


Umeona, Al Merrikh ya Sudan walikuwa wa kwanza kuonyesha nia ya kuhakikisha wanapata huduma ya Manula na Simba wanaonyesha nao wana jeuri ya fedha kwa kuwa bado wanamuhitaji.


Sasa kuna tetesi vigogo wengine wa Afrika, Mamelodi Sundowns sasa nao wanatupa jicho kwa Manula, tayari wameona Afrika Mashariki kuna asali baada ya huduma nzuri ya Denis Onyango ambaye wanajua baada ya muda mfupi ujao atatundika daruga.


Mamelodi wangeweza kuangalia kipa mwingine nchini Uganda lakini kama mwenye jicho amekwishatazama, ukweli haujifichi tena kwa kuwa Onyango anastaafu, wanaona mbadala anaweza kuwa Manula.


Kipa kuwa gumzo si jambo dogo, kipa kuwaniwa na timu kubwa si jambo la mzaha. Maana yake kuna jambo kubwa amelifanya na linapaswa kuwa funzo kwa makipa wengine wa hapa nyumbani.


Sauti ya hili la Manula iko juu sana, hauhitaji kuongeza. Kila mmoja anasikia vizuri sana na anaelewa kwamba kipa anaweza kununuliwa kwa bei kubwa na kupata mshahara bora kabisa.


Zile hisia za zamani kwamba mshambuliaji, kiungo au beki pekee ndiyo wanaweza kununuliwa kwa fedha nyingi limepitwa na wakati. Kila mmoja anaweza kula kwa urefu wa kamba yake yake. Inategemea tu ni aina gani ya kamba.


Manula ameifanya kazi yake kwa juhudi kubwa, amejifunza kutokana na makosa ya misimu mitatu mfululizo. Hakukataa pale alipoelezwa hata alipokwazika na leo ndiyo ubora alionao na thamani imepanda kwa kiwango cha juu sana.


Wale ambao walikuwa wanambeza wanaweza

kujifunza kwake, wale waliomsema kwa nia ya

kumfanya abadilike wanaweza kujivunia lakini

makipa, wanaweza kumtumia kama mfano wa

kubadilisha maisha yao ya kazi na kupiga hatua

kimaisha.


Unaweza kusema Manula ameibua tena nafasi ya makipa na inawezekana leo anakuwa ushawishi kwa watoto na vijana ambao walidhani kuwa kipa ni hasara na sasa watavutiwa zaidi kucheza kwa juhudi na maarifa kutafuta ubora.


Kumchukulia Manula kama faida, kuna uwezekano mkubwa wa kufaidika zaidi. Kumchukulia kishabiki au kukasirishwa na maendeleo yake ni kujiumiza tu mwenyewe na kupoteza muda.