Home Simba SC WACHEZAJI SIMBA KUZOA MILIONI 600 WAKIIFUNGA AS VITA LEO

WACHEZAJI SIMBA KUZOA MILIONI 600 WAKIIFUNGA AS VITA LEO


UNAAMBIWA Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Simba, ambaye pia ni mwekezaji wa klabu hiyo, Mohamed Dewji ‘Mo’, ameamua kuichukulia mechi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya AS Vita kama fainali na kuna mzigo ambao umetengwa.

 Taarifa za ndani zinadai kuwa hadi kufikia sasa kuna mamilioni ya fedha yametumika na mengine yatatumika ambapo jumla ni shilingi milioni 600 ili kuongeza motisha kwa wachezaji na benchi la ufundi kama watafanikiwa kuvuna pointi tatu.

Leo, Simba inatarajiwa kushuka kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam, kuwakabili AS Vita Club ya DR Congo kwenye mchezo wa marudio ikiwa na kumbukumbu ya kuvuna pointi tatu kwenye mechi ya kwanza ya ugenini.

Simba ndiyo kinara wa Kundi A kwa kuwa na pointi 10, ilizozikusanya baada ya kucheza dhidi ya AS Vita ugenini, Al Ahly ya Misri nyumbani, Al Merrikh ya Sudan nyumbani na ugenini pia.

Habari zimeeleza kuwa tayari marafiki wa Mo, ambao nao ni watu wenye fedha, wamekuwa wakichanga kila kunapokuwa na mechi muhimu na wameshamuahidi katika mchezo huu kuwa watachangia katika fedha atakazowapa benchi la ufundi na wachezaji.

“Kwa ahadi ambayo nimeisikia kutoka kwa bosi wetu Mo, hadi sasa sina shaka juu ya wachezaji wetu kuvuna pointi tatu mbele ya AS Vita, maana tajiri tayari ameshaunganishiwa nguvu na marafiki zake.

“Bosi hataki utani kabisa kwenye mchezo huo, kwani amesema ni bora watumie fedha nyingi kutoa motisha kwa wachezaji ili washinde hapa nyumbani na siyo kusubiria kule Misri ambako naamini kama tukikosa uhakika wa ushindi hapa itakuwa ngumu sana kupata pointi tatu au moja tunayohitaji ili tusonge mbele,” kilisema chanzo hicho.

Chanzo: Championi

SOMA NA HII  MCHAMBUZI:- CHAMA HANA CHAZIDIA ATAKACHOWAPA SIMBA...WAACHANE NAYE TU...