Home Azam FC YANGA V AZAM FC KWA MKAPA LEO KITAUMANA

YANGA V AZAM FC KWA MKAPA LEO KITAUMANA

 


REKODI zinaonesha kwamba, Oktoba 15, 2008, ilikuwa mara ya kwanza Yanga kukutana na Azam kwenye Ligi Kuu Bara ambapo matokeo ya mchezo huo, Yanga iliikaribisha vizuri Azam kwenye michuano hiyo kwa kuichapa mabao 3-1.

 

Huo ndiyo ulikuwa msimu wa kwanza kwa Azam kucheza Ligi Kuu Bara. Leo Jumapili, timu hizo zinakutana tena Uwanja wa Mkapa, Dar, ukiwa ni mchezo wa 26 ndani ya ligi hiyo.

 

Safari hii ushindani unatarajiwa kuwa mkubwa zaidi vijana wanasema leo kitaumana kutokana na nafasi za timu hizo kuelekea mechi za mwisho za kumalizia msimu huu wa 2020/21.


Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Azam Complex, Dar, Yanga ilishinda 1-0, mfungaji akiwa Deus Kaseke dakika ya 48.


Wakati ule, Benchi la Ufundi la Yanga liliongozwa na Cedric Kaze raia wa Burundi, huku lile la Azam likiongozwa na Mromania, Aristica Cioaba.

 

 Yanga yenye pointi 57, itataka kushinda mchezo wa leo ili kurudi kileleni mwa msimamo wa ligi hiyo, huku Azam yenyewe ikitaka ushindi kwa namna mbili; kupunguza wigo wa pointi dhidi ya Yanga na kulipiza kisasi kutokana na kupoteza mchezo wa kwanza nyumbani.


Katika mechi 25 zilizopita baina ya timu hizo kwenye Ligi Kuu Bara, Yanga imeshinda tisa, Azam nane na sare nane.

 

KAULI ZA MAKOCHA


Kocha wa Makipa wa Yanga, Razak Siwa, amesema: “Ni mechi ya ushindani ukizingatia wapinzani wetu Azam FC wanahitaji kulipa kisasi, sisi pia tunahitaji kupata pointi tatu.


“Wachezaji wapo fiti, lakini tunaweza kumkosa Tuisila Kisinda huyu ni asilimia 50/59 uwepo wake ama kutokuwepo,” .

 

Kocha Msaidizi wa Azam, Vivier Bahati, amesema: “Mechi ya kwanza tulipoteza nyumbani, sasa hatutakubali kupoteza tena, tutacheza kwa kuiheshimu Yanga na tutaingia kwa kutafuta matokeo mazuri,”.


SOMA NA HII  KISA KUSHINDWA KUMLIPA KOCHA....FIFA KUIZUIA YANGA KUFANYA USAJILI...ISHU NZIMA IKO HIVI..