BAADA ya kupoteza kwa kufungwa bao 1-0 dhidi ya Yanga kwenye mchezo wa Kombe la Shirikisho, wachezaji wa Prisons wameonekana kumshushia lawama mwamuzi wa kati wakidai kwamba hakuwasikiliza malalamiko yao.
Mwamuzi wa kati wa mchezo huo alikuwa ni Athuman Lazi ambaye alionekana akilalamikiwa na wachezaji wa Prisons wakiongozwa na nahodha Benjamin Asukile.
Ni bao pekee la Yacouba Sogne dakika ya 53 lilitosha kuwapaleka Yanga hatua ya robo fainali huku wakisubiri droo ipangwe ndio wajue timu ambayo watacheza nayo hatua ya robo fainali.
Asukile amesema kuwa hawakutendewa haki na mwamuzi kwa kuwa walikuwa na uwezo sawa na wapinzani wao ndani ya Uwanja wa Nelson Mandela ila refa hakuwa upande wao.
“Kwa upande wa mpira uwezo tulikuwa sawa ila kwa upande wa refa hakuwa upande wetu, wao walituzidi hapo kwa kuwa kila ambapo tulikuwa tukimfuata mwamuzi alikuwa akituambia hajaona, kuna penalti ambayo hatukupewa, bado mwamuzi alisema hajaona.
“Ikiwa mwamuzi hajaona basi inamaana yeye ni kipofu basi asingekuja kuchezesha mchezo wetu, tumeonewa na hatujatendewa haki,” aliongea Asukile.
Hivi karibuni kumekuwa na malalamiko kuhusu waamuzi kuchezesha chini ya kiwango jambo ambalo limekuwa lisababisha washindi wapatikane wale ambao hawajatarajiwa.
Katika mchezo huo uliochezwa Uwanja wa Nelson Mandela jumla ya kadi nne za njano zilionyeshwa na zote zilikwenda kwa Tanzania Prisons.
Kuhusu suala la waamuzi kuchezesha chini ya kiwango, Mwenyekiti wa Kamati ya Waamuzi, Sud Abdi Mohamed alisema kuwa huwa wanawapa elimu waamuzi na makosa ambayo wanayafanya kuna kamati maalumu ambayo huwajadili na kutoa adhabu kulingana na makosa hayo.