MABOSI wa Simba wameamua kuidhibiti mapema safu yao ya ulinzi hiyo ni baada ya kuwapa mikataba walinzi wake wengine wawili waliokuwa wakimaliza mikataba ambao ni Kennedy Juma na Erasto Nyoni tayari kwa kuivaa Yanga Mei 8, mwaka huu bila kinyongo.
Simba Jumamosi ijayo itakuwa mwenyeji wa Yanga katika mchezo wa Dabi ya Kariakoo pale Uwanja wa Mkapa, Dar katika mchezo wa mzunguko wa pili wa Ligi Kuu Bara.
Mpaka sasa Simba tayari imeshafanya uboreshaji wa mikataba ya wachezaji wake wa safu ya ulinzi ikianza na Mohamed Hussein ‘Tshabalala’, kisha Shomari Kapombe kisha ikashuka kwa Kennedy Juma na sasa inaelezwa imemalizana na Erasto Nyoni pia straika John Bocco naye ametia saini.
Kennedy Juma ambaye mkataba wake na Simba ulikuwa ukitarajiwa kufikia kikomo mwezi huu amekiri kuongeza tena kandarasi ya miaka miwili huku akidai bado kuna mazungumzo ya baadhi ya mambo ndani ya mkataba yanaendelea.
“Kweli mkataba wangu wa awali na Simba ulitarajiwa kuisha mwezi wa tano, hivyo tayari nipo kwenye mazungumzo na uongozi wangu kuhusiana na kuboreshewa baadhi ya mambo madogo tu, ila kimsingi mkataba mpya naweza kusema wazi tayari nimeshasaini na siwezi tena kwenda popote pale,” alisema Kenedy.
Aidha mkongwe, Nyoni naye anaripotiwa kumalizana na Simba hivyo Mei 8, atakiwasha kiroho safi bila hofu ya mkataba.
Chanzo: Championi