Home Ligi Kuu TUSIIGEUZIE TFF NCHA YA KISU WAKATI UKWELI TUNAUJUA

TUSIIGEUZIE TFF NCHA YA KISU WAKATI UKWELI TUNAUJUA

 


GUMZO kubwa kwa sasa katika mpira wa 
Tanzania ni kuahirishwa kwa mechi ya watani Simba na Yanga, mechi ambayo ilipangwa kuchezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam, juzi Jumamosi.


Mechi hiyo ilikuwa inasubiriwa kwa hamu, Simba wakitaka kujikita kileleni zaidi huku Yanga wakitaka kupunguza pengo la pointi nne kwa kuwa wao wanazo 57 na watani wao wana 61.


Kila shabiki alikuwa anaamini ni wakati mwafaka wa kikosi chake kufanya kweli, Simba wakijivunia ubora wa kikosi chao na Yanga wakielezea ubabe wao kwa Simba.


Ilikuwa ni raha ya ushindani karibu wiki nzima za tambo za watani wa jadi, mechi hiyo maarufu kama Kariakoo Dabi ambayo mwisho wake imeishia hewani.


Kilichosababisha mechi hiyo kuahirishwa ni agizo kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo na Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) kupitia Bodi ya Ligi Tanzania (TPLB) wakalitekeleza.


Agizo halikuwa kuahirisha mechi, agizo lilikuwa ni kusogeza mbele mechi kwa muda wa saa mbili pekee na baada ya hapo kipute kingepigwa. TFF na TPLB walipanga mechi ichezwe saa 11 jioni, lakini siku hiyohiyo wakapata agizo la wizara kwamba mechi hiyo itapigwa saa 1 usiku. Saa mbili mbele ya muda waliokuwa wamepanga.


TFF kupitia TPLB, wakawataarifu wadau wao Simba waliokuwa wenyeji na Yanga kwamba mambo yatakuwa hivi.

Wakayapokea lakini mwisho tumeona Yanga waliamua kutoa timu uwanjani tayari mashabiki wakiwa wameingia uwanjani mapema.


Maswali ni mengi sana, kwamba vipi wafunge safari hadi uwanjani na baada ya hapo watoe timu kwa kusogezwa saa mbili mbele? Kuna jambo gani linawafanya Yanga kuwa katika uamuzi huo, tuwaachie wenyewe kwanza na ninaamini watalimaliza vizuri ingawa busara ya kuangalia usalama wa mashabiki, haikuwa imetumika na badala yake ulikuwa uamuzi wa kishabiki.


Ukiachana na hilo vizuri tukaliangalia katika sura ya pili, kuwajalidi TFF ambao wamekuwa wakishambuliwa na kufikia hatua ya viongozi wao kudhalilishwa.


Najua wapo watu huona au kuamini silaha yao ni matusi, huamini kutukana ndio jambo sahihi au ndio ujengwaji wa hofu au ndio uchambuzi wa jambo fulani lakini ukweli ni hivi, unayeona anatukana tu, anakuwa na uwezo mdogo sana wa ufikiri.

SOMA NA HII  RATIBA YA MECHI ZA LIGI KUU BARA LEO


Hapa TFF unawalaumu wapi na kufikia kuwadhalilisha, agizo limetoka wizarani ambayo ni Serikali ya nchi yetu, wao wanaweza kupinga vipi? Lakini nani anajua Serikali iliamua hivyo kwa sababu zipi za msingi kwa kuwa kila mmoja anasema lake?

Kama ni suala la kiusalama je? TFF wanaweza vipi kuipinga Serikali? Katika taarifa yao, TFF wamesema

wamefikia uamuzi huo baada ya kupokea agizo kutoka Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo. Hii nayo haieleweki hadi watu kuelekeza ncha ya kisu kwao na kuwashambulia bila sababu za msingi.


Inawezekana ukawa fundi sana wa kulaumu, fundi sana wa matusi lakini basi jifunze hata kusoma na kuelewa halafu ukajenga hoja zako na watu wakakuelewa.

Yanga walifuata kanuni, TFF wakafuata agizo la Serikali, tujadili katikati ya hapo, nini kingetumika, weledi, busara, mihemko?

Lakini si mashambulizi tu kwa TFF kwa kuwa ndio mazoea. Vizuri kuifanya mijadala ya mchezo wa soka ikawa inayozalisha au kufundisha badala ya mihemko na kukurupuka kuwa ni sehemu ya mijadala ya mchezo wa mpira au kutengeneza picha eti watu wa mpira wako.