JOHN Bocco, nahodha wa Simba amesema kuwa wana kikosi bora jambo ambalo linawafanya wawe na imani ya kupata matokeo mbele ya Kaizer Chiefs kwenye mchezo wao wa Ligi ya Mabingwa Afrika unaotarajiwa kuchezwa Mei 15.
Bocco alikuwa ni miongoni mwa wachezaji 24 ambao walikwea pipa Mei 11 kuelekea Afrika Kusini kwa kupita Kenya kwa shirika la ndege la Kenya Airways aliliambia Championi Jumatano wana imani ya kufanya vizuri.
Ni Mei 15, Uwanja wa SA FNB Simba nayonolewa na Kocha Mkuu, Didier Gomes itakuwa na kazi ya kusaka pointi tatu kwenye robo fainali ya kwanza na ile ya pili itachezwa Mei 22, Uwanja wa Mkapa.
Bocco alisema:”Tuna kikosi imara kwa sasa na kila mchezaji anapenda kuona timu inapata matokeo hivyo tunawafuata wapinzani wetu tukiamini kwamba tunakwenda kusaka ushindi, mashabiki watuombee.
“Malengo yetu kushinda ili tuweze kufikia malengo ambayo tulikuwa tumejiwekea tangu mwanzo wa msimu hilo linawezekana na tunajua kwamba wapinzani wetu wapo imara ila hatuna mashaka tunawaheshimu,” .
Kwa sasa kikosi cha Simba kinaendelea na mazoezi nchini Afrika Kusini kwa ajili ya kujiweka sawa kwa ajili ya mchezo huo unaotarajiwa kuwa na ushindani mkubwa.