KOCHA Mkuu wa JKT Tanzania, Abdalah Mohamed, ‘Bares’ amesema kuwa wachezaji wake walipata nafasi na kushindwa kuzitumia mbele ya Yanga kwenye mchezo wao wa Ligi Kuu Bara uliochezwa jana, Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.
Pia ameongeza kuwa safu yake ya ulinzi imeruhusu mabao mepesi jambo ambalo limewafanya wapoteze pointi tatu.
Bares amesema:”Ninawapongeza vijana wangu kwa kupambana ila mabao ambayo tumefungwa ni mepesi hasa kutokana na kukosa mawasiliano kwa safu ya ulinzi pamoja na umakini kwa washambuliaji.
“Nafasi moja ambayo tuliipata kipindi cha kwanza nina amini kwamba tungeitumia vizuri ingetupa nafasi ya kutulia na kufanya vizuri katika mchezo wetu.
“Kipindi cha pili mechi JKT Tanzania tuliikamata kidogo ila tumepoteza na tunatazama mchezo ujao kwa sababu makosa tumeyafanya mengi.
“Mechi nne ambazo tumebakiwa nazo bado hakuna tatizo kwa kuwa nina amini kuwa Mungu atatusaidia na tutafanya vizuri.,”.
Kwenye msimamo wa Ligi Kuu Tanzania Bara, JKT Tanzania ipo nafasi ya 14 imekusanya pointi 33 baada ya kucheza jumla ya mechi 30, Yanga ipo nafasi ya pili na ina pointi 61 baada ya kucheza jumla ya mechi 29.