KUNA jambo haliko sawa Yanga, ndiyo kuna jambo haliko sawa hata kama uongozi wa kikosi cha klabu hiyo utakuwa hautaki kuliweka wazi, lakini vipo viashiria vingi kuwa kuna kitu Uongozi wa Yanga unapaswa kukifanya ili kuirejeshea timu hiyo makali yake.
Ndani ya michezo 18 ya kwanza msimu huu, Yanga ndiyo ilikuwa timu ambayo inahofiwa zaidi kwenye Ligi Kuu Bara, Yanga ilikuwa timu inayocheza kwa umoja na ari ya hali ya juu.
Morali hii iliwafanya Yanga wawe tishio licha ya upya wa nyota wengi ambao walikuwa wanaanza ndani ya kikosi chao.
Yanga hawakuwa na muunganiko wa kitimu uwanjani ‘Chemistry’ kiasi cha kugharimu kibarua cha aliyekuwa kocha wa kwanza wa kikosi cha timu hiyo msimu huu, Zlatko Krmpotic baada ya kuiongoza katika michezo mitano tu.
Lakini licha ya yote haya, bado Yanga walikuwa wakipata matokeo chanya uwanjani. Lakini vipi kuhusu michuano ya kombe la Mapinduzi?
Yanga walikaza kamba katika michuano hiyo iliyofanyika mapema mwaka huu na kufanikiwa kumaliza ukame wa misimu mitatu bila kikombe chochote, baada ya kutwaa ubingwa huo tena mbele ya mtani wao Simba walioingia nao fainali na kuwafunga kwa penalti 4-3.
Katika hali ya kushangaza baada ya ubingwa wa kombe la Mapinduzi, Yanga katika michezo sita mfululizo ya Ligi kuu iliyofuata walipata ushindi katika mchezo mmoja pekee, wakipoteza dhidi ya Coastal Union na kutoa sare michezo minne.
Nikukumbushe tu kuwa mchezo dhidi ya Coastal ulioisha kwa Wananchi kukubali kipigo cha mabao 2-1 ndiyo ulikuwa mchezo wa kwanza Yanga kupoteza msimu huu, hivyo kumaliza ‘unbeaten’ yao ya michezo 21.
Tangu hapo ndani ya kikosi cha Yanga vimbwanga vingi vikaanza kujitokeza kiasi cha kugharimu vibarua vya benchi lote la ufundi lililokuwa likiongoza na kocha Mrundi, Cedric Kaze na wasaidizi wake.
Mwambusi aliyeachiwa kikosi akafanya mabadiliko yake kama kocha, lakini bado kukaonekana kuna kitu ambacho hakijakaa sawa, unakumbuka kilichotokea kati ya Deus Kaseke na Saido Ntibazonkiza kwenye mchezo dhidi ya Gwambina?
Hivi karibuni Haruna Niyonzima, Fiston Abdulazack na Lamine Moro wote katika nyakati tofauti, wameonekana kuiingia kwenye sintofahamu zisizo na afya kwa kikosi cha Yanga.
Mfululizo wa matukio haya unaonyesha wazi kuwa kuna mahali hakujakaa sawa katika mfumo wa uendeshaji wa timu yao.
Yanga wameporomoka kutoka katika uongozi wao wa msimamo kwa takribani miezi saba mpaka katika nafasi ya pili ambayo pia Azam wanaonekana ‘kuinyapianyapia’.
Nadhani kwa masilahi mapana ya klabu hii yenye historia kubwa na mashabiki lukuki hapa nchini, uongozi wa Yanga haupaswi kuficha changamoto inayowasumbua bali waiweke wazi na kuhakikisha wanaimaliza mapema kabla timu hiyo haijapoteza muelekeo kabisa.
Ntibanzokiza yeye aliomba kubadilishwa kwenye mchezo wa ligi baada ya kuonekana kuwa hakupenda kuanzia benchi ila mwisho wa siku ilikuwa ni funika kombe mwanaharamu apite kwa kuwa aliongea kwamba ilikuwa ni sehemu ya mchezo.
Niyonzima hivi karibuni ilielezwa kuwa anahitaji kusepa ndani ya kikosi hicho ila mwisho ikaja kuelezwa kuwa ni tetesi hazina ukweli.
Hakuna namna ikiwa kuna ukweli na unafichwa ipo siku kila kitu kitakuwa wazi na lile lililofichwa litagundulika tu.