KATIKA kuhakisha Simba inafanikiwa kupata ushindi dhidi ya Kaizer Chiefs katika mchezo wa marudiano wa Robo Fainali ya Ligi ya Mabingwa Afrika, Kocha Mkuu wa Simba, Didier Gomes ametumia muda wake kufundisha kuhusu kucheza mipira ya juu ambayo imeonekana kuwa tatizo katika mchezo wa kwanza uliofanyika nchini Afrika Kusini.
Simba katika mchezo wa awali wakiwa ugenini walipoteza kwa kufungwa mabao 4-0 ambapo mchezo wa marudiano unatarajiwa kufanyika kesho Jumamosi kwenye Uwanja wa Mkapa, Dar.
Katika mazoezi ya mwisho kufanywa na Simba mbele ya mashabiki kwenye Uwanja wa Mo Simba uliopo Bunju, Dar es Salaam, Kocha Gomes aliwatenga mabeki wa pembeni wa timu hiyo na washambuliaji kisha kuwafanyisha mazoezi ya kupiga krosi na washambuliaji kufunga jambo ambalo ni taswira ya kile ambacho wataenda kukifanya dhidi ya Kaizer Chiefs.
Mabeki wa pembeni ambao walikuwa wakipiga krosi walikuwa ni Shomari Kapombe, David Kameta, Mohamed Hussein na Gadiel Michael huku washambuliaji ambao walikuwa wakimalizia krosi hizo ni Chris Mugalu, Meddie Kagere na John Bocco kisha baadaye waliongezeka Clatous Chama na Luis Miquissone.
Aidha, katika mazoezi hayo mshambuliaji Mugalu ndiye alikuwa kinara wa kutupia mabao mengi ambapo alifanikiwa kufunga mabao 11 kati ya krosi 17 ambazo alipigiwa katika pande zote mbili za kushoto na kulia.
Washambuliaji Meddie Kagere na John Bocco wote walifanikiwa kufunga idadi sawa ya mabao wakifunga 10, ambapo Bocco alifunga mabao hayo katika krosi 16 alizopigiwa huku Kagere yeye akifunga idadi hiyo katika krosi 17 alizopigiwa.
Kwa upande wa asisti beki wa kushoto, Mohamed Hussein ‘Tshabalala’ ndiye aliyekuwa kinara wa pasi za mabao ambapo alifanikiwa kutoa asisti 10 huku Kapombe akitoa 9, Gadiel alifanikiwa kutoa pasi 7 huku Kameta akifanikiwa kutoa pasi 5 za mabao.
Aidha, Gomes alionekana akiwasisitizia mabeki wa timu hiyo kupiga krosi za aina yote za juu na chini kwa ufasaha ili kuhakikisha kuwa wanapata mabao ya aina yote kuelekea mchezo huo.