NYOTA wa kikosi cha Yanga, Carlos Carlinhos hali yake imeanza kurejea kwenye ubora wake na huenda akawa tayari kuwavaa wapinzani wao Mwadui FC.
Kwa sasa kiungo huyo raia wa Angola alikosekana kwenye mechi kadhaa ikiwa ni pamoja na ile dhidi ya Namungo 0-0 Yanga na JKT Tanzania 0-2 Yanga.
Sababu kubwa iliyofanya asiwe miongoni mwa wachezaji hao ni majeraha ya misuli ambayo aliyapata kwenye mchezo wa hatua ya 16 bora dhidi ya Tanzania Prisons uliochezwa Uwanja wa Nelson Mandela ambapo ubao ulisoma Prisons 0-1 Yanga.
Habari kutoka ndani ya Yanga zimeeleza kuwa tayari Carlinhos amesharejea kwenye ubora wake jambo ambalo limemfanya Kocha Mkuu, Nassredine Nabi kuomba ajumuishwe kikosini.
“Nabi amepata taarifa kwamba Carlinhos yupo fiti hivyo anahitaji kumuona ndani ya kikosi ili aanze program kwa ajili ya mechi zijazo.
“Ikiwa ataanza mazoezi basi anaweza kuanza kwenye mchezo ujao dhidi ya Mwadui FC kwa kuwa anakubali uwezo wake,” ilieleza taarifa hiyo.
Ofisa Habari wa Yanga, Hassan Bumbuli amesema kuwa wachezaji ambao wanasumbuliwa na majeraha hali zao zinaendelea salama.