NYOTA wawili wa Simba ambao walikuwa nje kwa muda wakipewa matibabu kutokana na majeraha yao ambayo waliyapata wakati wakitimiza majukumu yao wamerejea kikosini na kuanza mazoezi.
Ni beki wa kati Joash Onyango na mkata umeme Taddeo Lwanga ambao hawa kwa pamoja Mei 22 waligongana na kupata maumivu wakati wakipambana mbele ya Kaizer Chiefs kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika uliochezwa Uwanja wa Mkapa.
Wachezaji hao ambao ni chaguo la kwanza la Kocha Mkuu, Didier Gomes hawakumaliza dakika 90 kwenye mchezo huo na kumlazimu kocha huyo kufanya mabadiliko ya lazima.
Katika mchezo huo Simba ilishinda kwa mabao 3-0 Kaizer Chiefs, ila ilishindwa kutinga hatua ya nusu fainali kwa sababu mchezo wa kwanza ilipoteza kwa kufungwa mabao 4-0 nchini Afrika Kusini.
Jana Uwanja wa Mo Simba Arena walianza mazoezi pamoja na wachezaji wengine ikiwa ni kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wa leo wa Kombe la Shirikisho dhidi ya Dodoma Jiji.
Mchezo huo unatarajiwa kuchezwa Uwanja wa Mkapa majira ya saa 1:00 usiku ambapo ikiwa Gomes ataamua kuanza nao kikosi cha kwanza kama ataona inafaa anaweza kufanya hivyo kwa mujibu wa Ofisa Habari wa Simba, Haji Manara.