Home Yanga SC ISHU YA LAMINE MORO NA YANGA IMEFIKIA HAPA

ISHU YA LAMINE MORO NA YANGA IMEFIKIA HAPA


 MABOSI wa Yanga imeelezwa kuwa kwa sasa wamefikia maamuzi mazuri na beki wa kati ambaye ni nahodha Mghana, Lamine Moro na kumrejesha kikosini.

Hiyo ikiwa ni siku chache tangu beki huyo aondolewe kwenye kikosi cha timu hiyo na Kocha Mkuu wa Yanga raia wa Tunisia, Nasreddine Nabi kwa kile kilichoelezwa utovu wa nidhamu.

Beki huyo aliondolewa akiwa Ruangwa, Lindi wakati timu hiyo ilipokwenda kucheza mchezo wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Namungo FC kwenye Uwanja wa Kassim Majaliwa.

Akizungumza na Championi Ijumaa, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa timu hiyo, Hassan Bumbuli, alisema kuwa uongozi wa Yanga umefikia muafaka mzuri na beki wake baada ya wiki iliyopita kukaa naye kikao na kusikiliza madai yake.

Bumbuli alisema kuwa uongozi ulifanya kikao na beki huyo kwa ajili ya kusikiliza utetezi wake kutokana na kosa alilolitenda ambalo limefichwa, kabla ya kumsamehe.

Aliongeza kuwa, tofauti hizo mbili kati ya kocha na Lamine wamezimaliza na beki huyo atajiunga na timu mara baada ya kurejea juzi

Jumatano jijini Dar wakitokea kucheza mchezo wa robo fainali ya Kombe la FA dhidi ya Mwadui ambao ulimalizika kwa Yanga kushinda mabao 2-0.

“Isingekuwa vizuri uongozi kuchukua maamuzi ya kumuondoa kabisa kikosini Lamine bila ya kumsikiliza yeye, hivyo uongozi wiki iliyopita ulimuita na kufanya naye kikao kwa lengo la kusikiliza utetezi wake.

“Hiyo ni baada ya tatizo hilo kutokea kambini ambako hawakuwepo viongozi, hivyo tulimsikiliza kocha na wiki iliyopita tulimsikiliza Lamine utetezi wake, hivyo suala hilo tumelimaliza salama,” alisema Bumbuli.

“Baada ya kumaliza tatizo hilo, uongozi ulimbakisha hapa Dar kutokana na kutokuwepo katika mipango ya kocha kuelekea mchezo wetu wa FA dhidi ya Mwadui FC tuliocheza Uwanja wa CCM Kambarage, Shinyanga.”


SOMA NA HII  YANGA WAPEWA MBINU YA KUPINDUA MEZA KIBABE LEO KIMATAIFA