MABOSI wa Simba wameendelea kuwaongezea mikataba wachezaji wao baada kumpa mkataba wa miaka miwili beki Kennedy Juma huku kipa Beno Kakolanya wakiendelea kuvutana upande wa masilahi.
Habari kutoka ndani ya klabu hiyo zinaeleza kilichobaki kwa mchezaji huyo ni kutangazwa kwani kila kitu juu ya mkataba kipo tayari.
“Kennedy amemalizana na Simba kila kitu, bado kutangazwa tu na sababu kubwa iliyomfanya abaki ni uwezo wake mkubwa,” kilisema chanzo hicho
Kennedy alisajiliwa Simba misimu miwili iliyopita akitokea Singida United na alipoingia Simba licha ya kutopata nafasi ya kucheza mara kwa mara amekuwa akitumia vizuri nafasi anayopata.
Beki huyo katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Kaizer Chiefs uliochezwa wiki iliyopita akichukua nafasi ya Joash Onyango, Simba ikishinda 3-0 alionyesha uwezo mkubwa katika kupambana na washambuliaji wa Kaizer.
Kocha mkuu wa Simba, Didier Gomes amekuwa akimpa nafasi ya kucheza kama mbadala wa Pascal Wawa na Onyango, huku beki Ibrahim Ame akikosa nafasi kikosini humo.
Katika hatua nyingine, kipa wao Beno ambaye pia anamaliza mkataba wake ameanza mazungumzo na mabosi wake.
Habari zilizopo ni mabosi hao wamefanya mazungumzo na Meneja wa mchezaji huyo Seleman Haroub ingawa hawajamalizana.
“Mazungumzo yalifanyika kwa kifupi na kuonyesha tunahitaji kuendelea na mchezaji wake lakini kuna vitu kidogo vilifanya mazungumzo yasimalizike upande wa maslahi.”
“Meneja wake atazungumza tena na mmoja wa viongozi wetu ili kuweza kumalizana nae baada ya maongezi ya awali kutomalizika.”
Hata hivyo, Haroub alisema ni kweli mazungumzo yamefanyika; “Hatujamaliza, hivyo tukimaliza kila kitu kitawekwa wazi kama anabaki ama anaondoka kutokana na mapendekezo yetu.”
Kakolanya alijiunga Simba misimu miwili iliyopita akiwa mchezaji huru baada ya kumalizana na Yanga, alijiunga kuwa mbadala sahihi wa Aishi Manula ingawa bado hajaaminiwa kuwa kipa namba moja.