WAKATI Ligi Kuu Bara ikielekea ukingoni timu kubwa za Simba na Yanga zimeaanza maandalizi ya msimu ujao kimya kimya ili kuimarisha vikosi vyao.
Soka la Bongo limepata taarifa za uhakika kutoka ndani ya Yanga kuwa wapo kwenye harakati za kumsaini beki wa kushoto wa KMC, David Brayson.
Brayson amekuwa akiitwa katika kikosi cha Taifa Stars tangu akiwa kikosi cha Gwambina msimu uliopita aliposajiliwa na timu hiyo kwa mkataba wa mwaka mmoja ambao mwisho wa msimu huu unamalizika.
Taarifa hizo zinaeleza Yanga wapo kwenye hatua za mwisho kumsaini Brayson ili kuja kuwa chaguo la kwanza katika nafasi ya beki wa kushoto ambayo tangu ameondoka, Gadiel Michael hakuna aliyefiti kwa uhakika.
Wakati Yanga wakiwa kifua mbele kumnasa, Brayson Simba nao hawapo nyuma kwani walishafanya mazungumzo na mmoja wa watu wa karibu wa mchezaji huyo.
“Yanga wapo mbele zaidi kumpata Brayson ambaye mwisho wa msimu huu mkataba wake unamalizika, tumeongea nao na kukubaliana katika maeneo yote ya msingi,” alisema mtoa taarifa huyo.
“Simba ndio walikuwa wa kwanza kumfuata Brayson kwani walifikiri wanaweza kuachana na Mohammed Hussein ‘Tshabalala’ au Gadiel Michael aje kuchukua nafasi hiyo kama mbadala kwahiyo lolote linaweza kutokea,” alidokeza kiongozi mmoja mwenye ushawishi. Hata hivyo, Tshabalala aliongeza mkataba Simba.
Ofisa Mtendaji Mkuu wa KMC, Walter Harrison alisema; “Kwetu wala hatuna shida kama kuna timu ipo tayari kumchukua Brayson tutampa baraka zote kama ilivyokuwa kwa wachezaji wengine waliopita hapa, mpaka wakati huu katika ofisi yetu hakuna ofa rasmi.”
Brayson aliwafunga Yanga bao moja katika mchezo wa ligi uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa Aprili 10, katika sare ya bao 1-1.
Yanga kama watafanikiwa kumpata, Brayson maana yake kati ya Adeyun Saleh au Yassin Mustapha mmoja wapo anaweza kuachwa.
Yanga pia wapo sokoni kutafuta saini ya beki wa kulia ili kwenda kumuongezea nguvu, Kibwana Shomary lakini wapo katika mazungumzo ya karibu na mshambuliaji wa Dodoma, Dickson Ambundo.
METACHA IN, FARUK OUT
Katika hatua nyingine uongozi wa Yanga umepanga kuachana na wachezaji wao wa kigeni watano kutokana na viwango vyao ambavyo wameonyesha msimu huu.
Katika orodha hiyo ya wachezaji wa kigeni ambao wataachana nao yupo kipa, Faruk Shikhalo ambaye amekuwa si chaguo la kwanza.
Meneja wa Metacha, Jemedari Kazumari alisema kwa nyakati tofauti alizungumza na viongozi wa Yanga, Gharib Said, Senzo Mazingisa na Haji Mfikirwa.
“Wote kwa pamoja wameonyesha nia ya kumuongezea mkataba mpya Metacha na waliniambia mwanzoni mwa mwezi wa sita watamsaini mkataba mwingine huku wakimlipa kila kitu cha awali,” alisema Kazumari.