SASA rasmi mshambuliaji kipenzi cha Yanga, Mkongomani, Heritier Makambo anatua Jangwani baada ya kufikia muafaka mzuri.
Makambo ni kati ya wachezaji waliokuwepo kwenye mipango ya kusajiliwa na Yanga tangu msimu uliopita kabla ya dili lake kutokamilika na kuendelea kubaki kuichezea Horoya AC ya Guinea. Mshambuliaji huyo aliitumikia Yanga msimu wa 2018/19.
Kukamilika kwa dili hilo kunafanya jumla nyota watatu wawe wamemalizana na Yanga hadi hivi baada ya habari kueleza kuwa usajili wa wachezaji wawili ambao ni kiungo mshambuliaji wa Simba, Ibrahim Ajibu na beki wa KMC, David Bryson umekamilika.
Kuelekea msimu ujao, Yanga imepanga kukifanyia maboresho kikosi chake ikiwemo kufanya usajili kwenye safu ya ushambuliaji, kiungo na beki.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo Spoti Xtra,imezipata zimeeleza kuwa Yanga imefikia makubaliano hayo mazuri baada ya mshambuliaji huyo kuonesha nia ya kujiunga na timu hiyo.
Mtoa taarifa huyo alisema, Yanga tayari imefanya mawasiliano na viongozi wa Horoya ambao wenyewe wamekubali kumuachia mshambuliaji huyo aliyebakisha msimu mmoja kwenye mkataba wake wa kukipiga hapo.
Aliongeza kuwa, Yanga itaingia kwenye gharama ya kununua mkataba wa mwaka mmoja alioubakisha Horoya kama ilivyokuwa kwa Wakongomani, Mukoko Tonombe na Tuisila Kisinda walipojiunga na Yanga msimu huu.
“Makambo ni uhakika anarudi Yanga msimu ujao, ni baada ya yeye kuonesha nia, hivyo suala lipo kwa viongozi wa Yanga ndiyo wenye kibarua cha kuusitisha mkataba wake wa msimu mmoja uliobaki huko alipo.
“Hivi sasa kila kitu kinakwenda vizuri katika usajili wake, ni baada ya Yanga wenyewe kuwafuata Horoya ambao wameonekana kukubali kumuachia mshambuliaji huyo.
“Uzuri Makambo mwenyewe ndiye ameonesha nia ya kuja Yanga, atakuja na straika mwingine wa kimataifa,” alisema mtoa taarifa huyo.
Mtu wa karibu wa Makambo, amefichua ujumbe aliotumiwa na straika huyo uliosomeka: “Nimeimisi Yanga, Nimemisi Tanzania, ” .
Yanga kupitia Kocha Mkuu raia wa Tunisia, Nasreddine Nabi, alisema: “Nimepanga kukifanyia maboresho kikosi changu katika msimu ujao kwa kusajili wachezaji wenye uwezo watakaoisaidia timu kimataifa.”
.