IKIWA ni mechi nne kwa timu nyingi ndani ya Ligi Kuu Tanzania Bara zimebaki tunaona kwamba unakwenda kukamilika msimu huu wa 2020/21 ambao una ushindani mkubwa.
Kumalizika kwa msimu huu ni mwanzo wa maandalizi ya msimu mpya wa 2021/22 ambao unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa kuliko huu ambao umeonekana msimu huu.
Kiujumla ligi imekuwa na ushindani mkubwa, tangu mzunguko wa kwanza na sasa mzunguko wa pili unakwenda kukamilika huku kila timu ikivuna kile ambacho imepanda.
Licha ya kwamba kwa sasa ligi imesimama kutokana na maandalizi ya timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars kuelekea kwenye mchezo wa kirafiki dhidi ya Malawi, bado kuna timu zipo kambini zikiendelea na maandalizi ya mechi zao za lala salama.
Kwa upande wa wachezaji Stars ni lazima wachezaji wafanye kweli kwenye mchezo wao ili kupata matokeo mazuri pale ifikapo Julai 13.
Ushindani ndani ya ligi ya msimu huu umechangiwa kwa kiasi kikubwa na usajili ambao ulifanyika kwenye kila klabu inayoshiriki msimu huu.
Kwa sasa tayari timu zimejua mbivu na mbichi kama zilifanikiwa katika kuchanga karata zao juu ya usajili wao ama ziliambulia patupu hilo lipo wazi kwa sasa.
Kupitia matokeo ambayo yalitokea kwenye usajili uliopita ni wazi kwamba kwa sasa timu zitaanza kujipanga mapema kwa ajili ya usajili wa wakati ujao kwani muda tayari umekwishameguka.
Vita ya ubingwa itakwenda kukamilika muda si mrefu lakini haitakuwa na ushindani ikiwa timu nyingine zitakata tamaa na kuacha kuonyesha ushindani kwenye mechi zao ambazo zimebaki.
Kwa upande wa zile ambazo zinapambana kubaki ndani ya ligi ni wakati wao kuona namna gani wanaweza kutimiza malengo yao.
Zipo ambazo kwa sasa zimeona mwanga wa kubaki kwenye ligi na nyingine zinaishi kwa hisia kwamba zipo kwenye ligi huku akili zao zikiwa Ligi Daraja la Kwanza.
Kilichobaki kwa sasa ni kumaliza hesabu zile ambazo zilikuwa zimepangwa kwa sababu hakuna ambaye anahitaji kuona timu yake ikipoteza mechi ambazo itacheza.
Tayari mbili kutoka Ligi Daraja la Kwanza ambazo ni Mbeya Kwanza na Geita ni uhakika msimu ujao kuishi ndani ya Ligi Kuu Bara huku Mwadui FC wao wakiwa na uhakika wa kushiriki Ligi Daraja la Kwanza.
Kwa ambacho kimetokea basi ni muhimu kwa kila timu kwa sasa kuanza mipango makini hasa kuanzia kwenye usajili pamoja na kumaliza vema mechi zao ambazo zimebaki.
Pia ni muhimu kwa wachezaji kuwa na nidhamu katika kutimiza majukumu yao. Nidhamu ni muhimu kwa kila mchezaji iwe ni nje ya uwanja na ndani ya uwanja katika harakati za kusaka ushindi
Pia ninapenda pia kupongeza kuhusiana na mwamko mkubwa wa mashabiki wa soka hapa nchini ambao wamekuwa wakizidi kuwa na mapenzi makubwa na mchezo wa soka kila kukicha.
Ni muhimu hamasa hizi zikaendelea kuongezeka kwani kwa kufanya hivyo mashabiki wengi zaidi watahamasika kujitokeza uwanjani kuzishuhudia timu zao ambapo kiujumla mapato yatakayopatikana kupitia viingilio vyao yanaweza kuzisaidia timu zao kujiendesha kiuchumi.
Lakini pia viongozi wa mashabiki kwenye matawi mbalimbali hapa nchini wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kuwahamasisha wenzao ili kusapoti miradi mbalimbali ya klabu kama vile ununuaji wa jezi orijino za klabu zao.
Wachezaji wanapaswa kujitoa kwa hali na mali katika kusaka matokeo wasisahau kwamba Azam TV wanarusha matangazo yao duniani hivyo wapo sokoni.
Sio Bongo tu hata Zambia, Afrika Kusini nimekuwa nikiulizwa na marafiki zangu kuhusu mwendo wa ligi na namna ambavyo wanashuhudia kazi inavyokwenda.
Hii ni fursa kwa wachezaji kuweza kuwa sokoni kwa sababu mawakala wengi wanafuatilia ligi na kuona namna gani wanaweza kupata wachezaji kwa ajili ya kuwauza.
Muda huu kwa wachezaji ni fursa kwao na timu pia ni muhimu kupiga hesabu vizuri ili kupata wachezaji ambao watakuwa na manufaa kwao na sio kuwa mzigo wakati ujao.
Tunaona kwamba Azam FC wao wameanza kuwaongezea mikataba nyota wao ikiwa ni pamoja na Prince Dube, Ayoub Lyanga hili ni jambo la msingi.
Pia hata Simba nao wamefanya jambo zuri kwa kuwaongezea mikataba nyota wao ikiwa ni pamoja na Mohamed Hussein, Beno Kakolanya na John Bocco hivyo na wengine wanapaswa wafanye hivyo kwa wachezaji wao.