KIUNGO mchezeshaji, Salum Aboubakary ‘Sure Boy’ ataendelea kuichezea Azam FC katika misimu mingine miwili baada ya kuongezewa mkataba wa miaka miwili ya kuendelea kukipiga huko.
Awali, ilielezwa kuwa kiungo huyo yupo kwenye mipango ya kujiunga na Yanga katika msimu ujao kwa kile kilichodaiwa kugomea kuongeza mkataba Azam.
Taarifa ambazo imezipata Championi Ijumaa, kiungo huyo ameongeza mkataba wa miaka miwili kwa siri katika timu yake ya Azam utakaomalizika msimu wa 2023.
Mtoa taarifa huyo alisema kuwa wamemuongezea kiungo huyo mkataba kwa makusudi kwa hofu ya kuzidiwa ujanja na baadhi ya klabu kubwa za Simba na Yanga.
“Kama kulikuwa kuna timu ilikuwa inavizia saini ya Sure Boy, basi imekula kwao kwani mchezaji huyo ni mali yetu kwa misimu mingine miwili,” alisema mtoa taarifa huyo.
Alipotafutwa Ofisa Habari wa Azam, Thabiti Zakaria kuzungumzia hilo alisema: “Mbona mmechelewa kujua taarifa za Sure Boy kuongeza mkataba mpya? Sure ni mali yetu yupo hapa Azam hadi 2023.”