Home Taifa Stars MTEGO WA KUTOKUWA NA UZOEFU UKWEPWE LEO NA KIM MBELE YA MALAWI

MTEGO WA KUTOKUWA NA UZOEFU UKWEPWE LEO NA KIM MBELE YA MALAWI


VURUGU za usajili zimeanza taratibu japokuwa usajili wenyewe bado rasmi haujafunguliwa mpaka pale ligi itakapofika tamati. Baadhi ya timu zimeshaonyesha ni sehemu gani ambazo wataenda kusajili pale dirisha likifunguliwa.

Lakini pia kuna wachezaji tayari wameshaanza kufunga mabegi yao wakijiandaa kwenda katika makazi yao mapya ikiwa kwa kuhamia mazima baada ya kukubaliana na timu zao mpya katika vipengele kadhaa.


Yote haya ni mazuri kwa sababu naona msimu ujao wa ligi kuu kutokuwa na muda mrefu kuanza kwake baada ya msimu huu kumalizika, hivyo kuwapata mapema wale ambao mnawataka kutawapunguzia presha lakini pia itatoa muda mzuri kwa wachezaji kuunda  muunganiko wa timu.


Kushindwa au kuchelewa kusajili kutakuwa na athari kubwa sana kwa sababu kama nilivyosema nauona msimu ujao kuanza mapema tofauti na huu hivyo inaweza ligi kuanza kukawa na tatizo la wachezaji kutojuana kwa undani na jinsi wanavyocheza.


Tuliona baadhi ya timu zimefeli msimu huu kwa sababu zilifanya kosa kama hilo la kusajili, wengine walichelewa na wengine walijaza rundo la wachezaji lakini wakajikuta wanaishia pabaya kwa kuwaacha dirisha dogo baada ya kuona hawawezi kuwasaidia hata kidogo.


Mwisho wa yote tunataka kuona usajili ambao utakuwa salama, uliojaa ufundi na usio na mihemko ya namna yoyote ile kwa sababu kama timu itashindwa kufanya namna hiyo basi itakuwa inajichimbia shimo la kutumbukia yenyewe.


Timu ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars, leo hii Juni 13 inatarajiwa  kuwa na mechi ya kirafiki ya kimataifa mbele ya Malawi ambayo itapigwa katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar.


Mchezo huu umekuja kwa wakati na upo kwenye ratiba ya Shirikisho la Soka la Kimataifa (Fifa) ambapo utakuwa wa kwanza tangu Stars ichukuliwe na kocha Mdenishi Kim Poulsen.


Hii ni mechi muhimu kwa sababu itampa picha Kim ya namna gani kikosi hicho kipo tangu alipoondoka nchini na kurejea, atajua pia  arekebishe wapi na viwango vya wachezaji ambao amewaita ndani ya kikosi hicho atavitambua tu.

SOMA NA HII  HIZI HAPA 'MASHINE NANE ZA KIMATAIFA' ZINAZOIPIGANIA HESHIMA YA BENDERA YA TANZANIA...


Japokuwa ni mchezo ambao unahitaji kutafuta ushindi kwa ajili ya kuongeza pointi kwenye viwango vya dunia vinavyosimamiwa na shirikisho hilo lakini kuna kitu nataka kushauri kidogo.


Ingawa simfundishi Kim pamoja na benchi lake la ufundi nini cha kufanya lakini itapendeza kutoa angalau nafasi kwa wachezaji ambao hawana uzoefu na timu ya taifa kuweza kucheza mechi za namna hii kwa ajili ya kuwajenga zaidi.


Mara kwa mara tumekuwa tukilalamika kuwa wachezaji wengi wa hapa nyumbani hawana uzoefu na mechi za kimataifa hasa pale ambapo tunashiriki michuano ambayo haiwahusishi wachezaji wetu ambao wanacheza soka la kulipwa nje ya nchi.


Hivyo fursa hii iwe kwa wachezaji hao kwa ajili ya kuwajenga na kuwaonesha jinsi wanavyotakiwa kupambana pale ambapo watakapotakiwa kucheza mechi za kimataifa ili baadaye isije kuwa sababu kwamba tumefanya mashindano fulani kwa sababu wachezaji hawana uzoefu.