KOCHA Mkuu wa Yanga, Nasreddine Nabi imeelezwa kuwa anahitaji kumleta mchezaji ndani ya Yanga ambaye atatoka nchini Tunisia.
Hiyo yote katika kuhakikisha kikosi chao kinaimarika katika kujiandaa na michuano ya kimataifa msimu ujao ambayo Yanga huenda ikashiriki.
Yanga tayari imefanikisha usajili wa mabeki Shaban Djuma aliyemaliza mkataba AS Vita ya DR Congo na David Bryson wa KMC.
Kwa mujibu wa taarifa ambazo tumezipata kutoka ndani ya benchi la ufundi la timu hiyo, Kocha Nabi ndiye aliyependekeza usajili wa wachezaji wawili katika kukiimarisha kikosi hicho.
Mtoa taarifa huyo alisema kuwa, wachezaji hao ni chaguo lake kocha ambaye anaamini kama wakitua, basi wataisadia timu hiyo kutokana na uwezo na uzoefu wa kucheza michuano ya kimataifa.
Aliongeza kuwa, wachezaji hao aliowapendekeza ni kiungo mchezeshaji na mshambuliaji mmoja mwenye uwezo mkubwa wa kupachika mabao.
“Kocha Nabi amepewa majukumu yote ya kusimamia usajili kwa ajili ya msimu ujao, tayari amependekeza usajili wa wachezaji anaowahitaji.
“Nabi tayari ametoa mapendekezo ya usajili ukiwemo wa Bryson na Djuma baada ya kuridhishwa na uwezo wao.
“Pia kocha ametoa mapendekezo ya kusajili wachezaji wawili kutoka Tunisia, kati ya hao ni kiungo mchezeshaji na mshambuliaji mmoja,” alisema mtoa taarifa huyo.
Akizungumzia usajili wa Yanga, Mkuu wa Kitengo cha Habari na Mawasiliano wa timu hiyo, Hassan Bumbuli, alisema mipango yote ya usajili ipo kwa kocha ambaye yeye ndiye anahusika na kila kitu.