NAHODHA wa Simba John Bocco mfungaji bora wa Ligi Kuu Bara msimu wa 2011/12 akiwa anaichezea Azam FC na kumaliza msimu akifunga mabao 19 wakati Simba ikitwaa ubingwa kwa alama zao 62.
Juzi, Bocco alifungua kurasa ya mabao wakati Taifa Stars ikiichapa Malawi mabao 2-0 katika mchezo uliochezwa Uwanja wa Mkapa huku kazi kubwa ya upikaji mabao ikifanywa na Denis Kibu.
Bao hilo linamfanya Bocco kuwa na mwenendo mzuri wa kufunga mfululizo katika michezo mitano iliyopita ya timu Ligi Kuu pamoja na ule wa Azam Sport Federation (ASFC).
Mfululizo wa mabao yake alianza katika mchezo wa marudiano wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Kaizer Chief Uwanja wa Mkapa wakati Simba ikishinda mabao 3-0 huku Bocco akitupia mawili dakika ya 24 na 56 na bao lingine likifungwa na Clatous Chama.
Baada ya mchezo huo alikabidhiwa zawadi ya Sh 2,500,000 baada ya kuchaguliwa kuwa Mchezaji Bora wa mchezo huo huku akichaguliwa kuwa mchezaji bora wa wiki wa Ligi ya Mabingwa Afrika.
Katika mchezo wa robo fainali ya ASFC, alifunga mabao mengine mawili katika ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya Dodoma Jiji huku bao lingine likifungwa na Meddie Kagere.
Simba ikiwa kwenye Uwanja wa Majaliwa Mei 29 na Simba kushinda mabao 3-1 huku mshambuliaji huyo akifunga bao moja dakika ya 83 na mabao mengine yakifungwa na Chriss Mugalu pamoja na Benard Morrison.
Wakiwa Uwanja wa CCM Kirumba, Mwanza dhidi ya Ruvu Shooting, Simba iliendeleza ubabe wake kwa kuvuna alama tatu kwa ushindi wa mabao 3-0 na Bocco akifunga mabao mawili.