KIKOSI cha Simba jana Juni 19 kimeibuka na ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Polisi Tanzania kwenye mchezo wa ligi uliochezwa Uwanja wa CCM Kirumba.
Shukrani kwa Luis Miquissone ambaye alifunga bao pekee la ushindi dakika ya 28 kwa pigo huru ambalo lilimshinda mlinda mlango wa Polisi Tanzania Mohamed Yussufu.
Ushindi huo unaifanya Simba kusepa na jumla ya pointi 6 mazima mbele ya Polisi Tanzania ambapo kwenye mchezo wa kwanza uliochezwa Uwanja wa Mkapa ubao ulisoma Simba 2-0 Polisi Tanzania.
Licha ya Polisi Tanzania kupambana kusaka ushindi kwenye mchezo huo jitihada zao zilikwamia kwenye mikono ya kipa namba moja wa Simba, Aishi Manula ambaye alitimiza majukumu yake kwa umakini.
Alikuwa ni Tariq Seif wa Polisi Tanzania alikosa nafasi ya wazi kumtungua Manula kwa pasi ya Daruesh Saliboko dakika ya 7 pia dakika ya 72 Gerad Mdamu alifanya jaribio kwa kichwa ndani ya 18 likaokolewa na Manula.
Mzee wa kukera Bernard Morrison alionekana amekasirika baada ya kukosa kucheza mchezo wa jana kwa kuwa alikuwa kwenye benchi na alinyanyuliwa kwa muda ili kufanya mazoezi ila hakuweza kuingia na alionekana akipigapiga chupa za maji.
Sasa Simba imefikisha jumla ya pointi 70 baada ya kucheza mechi 28 wamebakiza mechi mbili ambazo ni sawa na dakika 180 ikiwa watashinda zote basi watatangazwa kuwa mabingwa kwa kuwa watafikisha jumla ya pointi 73 ambazo hazitafikiwa na wapinzani wao Yanga na Azam FC. ambao ni washindani wao wa karibu.