MCHEZAJI mkongwe, Erasto Nyoni ameahidi kugawa tiketi 50 kwa mashabiki wa Simba SC mjini Songea kwa ajili ya kuhudhuria mechi ya Kombe la Shirikisho (ASFC) dhidi ya Azam unaotarajiwa kuchezwa Jumamosi Juni 26 kwenye Uwanja wa Majimaji.
Nyoni ameamua kufanya hivyo ikiwa ni sabubu ya kuonyesha furaha kwa mashabiki zake na kuthamini mchango mkubwa kwa ndugu zake wa Songea ambao wamekuwa ni chachu ya mafanikio yake.
“Nimefurahi kurejea nyumbani baada ya muda mrefu nimefarijika sana kuonana na ndugu zangu, nawaahidi kutoa tiketi 50 za bure kwa mashabiki zangu kwa ajili ya mechi yetu dhidi ya Azam kwa kutambua mchango na umuhimu wao kwangu” alisema
Akizungumzia mchezo huo Nyoni alisema kuwa malengo yao ni kutetea taji hilo la shirikisho (ASFC) licha ya kutambua kuwa wanaenda katika mchezo huo ukiwa na taswira tofauti.
Alisema kuwa wanaenda kwenye mchezo huo kwa tahadhari kubwa kutokana na ubora mkubwa wa timu ambayo wanaenda kukutana nao.
“Azam ina wachezji wazuri ambao wanaweza kufanya lolote ni timu ambayo imekuwa ikitupa wakati mgumu pindi tunapokutana nayo, ingawa sisi kama wachezaji tumejipanga vyema kuhakikisha tunashinda mechi na kutimiza malengo yetu ya kulitetea tena kombe hil” alisema
Aidha alisema kuwa licha ya rekodi nzuri walizokuwa nazo katika uwanja wa Majimaji ila wao kama wachezaji hawatabweteka bali watapambana mpaka mwisho.
“Rekodi kwangu sio kipaumbele sana bali tunachoangalia kama wachezaji ni wakati uliopo tunafanya nini? Kwa maslahi mapana ya timu na mashabiki zetu kiujumla ambao wamekuwa wakitupa sapoti ya kutosha” alisema
Katika michezo mitano iliyopita Simba imeshinda michezo mitatu huku ikitoka sare katika michezo miwili kwenye uwanja wa Majimaji.