Home Simba SC AVEVA AFUNGUKA SABABU PESA ZA MAUZO YA OKWI KUWEKWA KWAKE

AVEVA AFUNGUKA SABABU PESA ZA MAUZO YA OKWI KUWEKWA KWAKE


Aliyekuwa rais wa Klabu ya Simba, Evans Aveva, amedai mahakamani kuwa Sekretarieti ya klabu hiyo ndio ilipendekeza dola za kimarekani 319,212 ziwekwe katika akaunti maalum na hivyo ukafanyika mchakato wa kufungua akaunti nyingine.

Fedha hizo zilitokana na mauzo ya mchezaji Emmanuel Okwi kwenda klabu ya Etoile du Sahel ya Tunisia.

Aveva ameeleza hayo jana, Jumanne, Juni 29, 2021 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakati akitoa utetezi wake.

Aveva ametoa utetetezi wake,  baada ya mahakama hiyo kuwakuta na kesi ya kujibu yeye na wenzake wawili, baada ya upande wa mashtaka kufunga ushahidi wao.

Mbali na Aveva, washtakiwa wengine katika kesi hiyo ya jinai ni aliyekuwa Makamu raisi wa klabu hiyo, Godfrey Nyange maarufu Kaburu na aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili wa Klabu hiyo, Zacharia Hans Poppe.

Washtakiwa kwa pamoja wanakabiliwa na mashtaka nane yakiweno ya kughushi nyaraka na matumizi mabaya ya madaraka kwa kuhamisha fedha za klabu bila kamati tendaji ya Simba kukaa kikao.

Akiongozwa kutoa utetezi wake na wakili wa Utetezi, Kung’e Wabeya, mbele ye Hakimu Mkazi Mkuu, Thomas Simba,  Aveva amedai kati ya mwaka 2014 hadi 2017, klabu ya Simba ilipata dola za kimarekani 319,212 ambazo zilitokana na mauzo ya mchezaji Emmanuel Okwi kwenda klabu ya Etoile du Sahel ya Tunisia.

Amedai kuwa baada ya kupokelewa kwa fedha hizo, yeye kama raisi wa klabu kipindi hicho,  aliitisha kikao cha kamati tendaji ili kutanabaisha matumizi ya fedha hizo na ikaamuliwa zitumike katika ujenzi wa Kiwanja Bunju, na Dola 17,000 alipwe aliyekuwa mwenyekiti wa kamati ya usajili Zachariah Hans Pope alizokuwa akiidai klabu hiyo.

Amedai kuwa Sekretarieti ya klabu ndio ilipendekeza fedha hizo ziwekwe katika akaunti maalum na hivyo ukafanyika mchakato wa kufungua akaunti nyingine.

” Zoezi la kufungua akaunti hiyo lilishindikana hivyo nikaombwa fedha hizi zihamishiwe katika akaunti yangu  binafsi.” Amedai Aveva na kuongeza

“Mheshimiwa hakimu mimi kama kiongozi Mkuu wa klabu nilikubaliana na ombi hilo lakini nilitoa sharti kwamba lazima kuandaliwe memorandum of understanding  kuhusu suala hilo,iliandaliwa na ikasainiwa na watu watatu ambao ni mimi rais wa klabu, makamu wa rais Geofley Nyange (Kaburu) na Katibu Mkuu ambaye pia alikuwa Mhasibu wa klabu Amos Gaumeni” ameeleza.

SOMA NA HII  SIMBA YATELEKEZWA NA MASHABIKI WAKE MECHI NA IHEFU...MAMA NTILIE WAGEUKA MASHABIKI

Hakimu Simba baada ya kusikiliza utetezi huo amehirisha kesi hiyo hadi Julai 12, 2021 itakapoendelea kwa mshtakiwa huyo kujitetezi.

Washtakiwa wangine wanatetewa na wakili Benedict Ishabakaki na Augustina Shio.

Kati ya mashtaka nane yanayowakabili, lipo  la kughushi linawakabili washitakiwa wote, ambapo wanadaiwa kughushi hati ya malipo ya kibiashara ya Mei 28, 2016 wakionyesha kwamba nyasi bandia zilizonunuliwa na Simba zinathamani ya dola 40,577 sawa na zaidi ya Sh milioni 90 huku wakijua kwamba sio kweli.

Shtaka jingine, inadaiwa Aveva, Nyange na Hans Poppe kati ya Machi 10 na Septemba 30, 2016 waliwasilisha nyaraka za uongo kuonyesha Simba imenunua nyasi bandia zenye thamani ya Dola za Kimarekani 40,577.