Home Ligi Kuu NAMNA YANGA WALIVYOPINDUA MEZA KIBABE MBELE YA MWADUI FC

NAMNA YANGA WALIVYOPINDUA MEZA KIBABE MBELE YA MWADUI FC


YANGA jana iliibuka na ushindi wa mabao 3-2 dhidi ya Mwadui FC kwenye mchezo wa Ligi Kuu Bara uliochezwa Uwanja wa Mkapa baada ya kupindua meza kibabe.


Mwadui FC ambao wameshashuka daraja walianza kupachika bao la kuongoza dakika ya 7 kupitia kwa  Aniceth Revocatus kwa kichwa matata kilichomshinda mlinda mlango, Faroukh Shikhalo ambaye hakuwa na chaguo.

Bao hilo lilidumu kwa muda wa dakika 15, liliwekwa usawa na Bakari Mwamnyeto ambaye ni beki wa kati kwa pasi ya kiungo, Saido Ntibanzokiza ambaye alipiga mpira wa adhabu akiwa nje ya 18 hili ni bao la tatu kwa beki huyo, huku mshambuliaji Fiston Abdulazack akiwa amefunga bao moja msimu huu.

Kipindi cha kwanza kilikamilika kwa ubao wa Uwanja wa Mkapa kusoma Yanga 1-1 Mwadui FC, ambayo ipo nafasi ya 18 kwenye msimamo wa ligi na haina uhakika wa kushiriki Ligi Kuu Bara msimu ujao.

Nyota wao Fiston atajilaumu yeye mwenyewe kwa kuwa alikosa penalti dakika 44, iliyookolewa na kipa namba moja wa Mwadui Mussa Mbissa ambaye alifanya kazi nzuri kwenye mchezo huo.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi ambapo Yanga walijitahidi kutafuta bao ikawa kazi kubwa kwao na mzigo wa pili wakabebeshwa na yuleyule Revocutus dakika ya 66 akiwa nje ya 18 kwa shuti kali  lililomshinda Shikhalo.  

Ngoma ilipinduliwa na Yacouba Songne dakika ya 90+1 na mmaliziaji alikuwa ni Wazir Junior ambaye alipachika bao la ushindi dakika ya 90+4 na kuipa pointi tatu mazima Yanga.

Ushindi huo unaifanya Yanga kufikisha jumla ya pointi 67 ikiwa nafasi ya pili baada ya kucheza mechi 31 huku Mwadui FC ikiwa nafasi ya 18 na pointi zake ni 19 baada ya kucheza jumla ya mechi 32. 

SOMA NA HII  HIZI HAPA SABABU 5 KUNTU KWA NINI MSUVA ATAJIUNGA NA YANGA NA KUIPIGA CHINI SIMBA...