Home news TAKUKURU WATHIBITISHA KUMSHIKILIA MANJI TOKA JUZI

TAKUKURU WATHIBITISHA KUMSHIKILIA MANJI TOKA JUZI


Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), imethibitisha kuwa inamshikilia mfanyabiashara Yusuph Manji kwa mahojiano.

Manji, ambaye aliondoka nchini mwaka 2018 baada ya Serikali kuondoa nia ya kuendelea na kesi iliyokuwa ikimkabili, amerejea juzi jioni na baada ya kukamilisha taratibu za uhamiaji akachukuliwa na maofisa wa Takukuru.

Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Kamishna wa Polisi Salum Hamduni ameliambia gazeti la Mwananchi kuwa wanamshikilia Manji kutokana na tuhuma tatu zinazomkabili.

Hamduni amesema kabla ya Manji kutoroka nchini kuna uchunguzi ulifanywa kuhusu kampuni zake za Intertrade Commercial Ltd Services na Golden Globe International Services Limited.

“Walikuwa wanafanya biashara na Tanesco (Shirika la Umeme Tanzania) kati ya mwaka 2011 na 2015. Anatuhumiwa kuisababishia hasara Serikali kwa kukwepa kodi ya VAT (Ongezeko la Thamani) na udanganyifu,” amesema Kamishna Hamduni.

Pia, amesema kupitia kampuni ya Golden Globe inadaiwa kuna udanganyifu ulifanyika wakati wa kununua hisa za kampuni ya mawasiliano ya Tigo ambayo tayari imeshauzwa kwa kampuni nyingine ya mawasiliano ya Madagascar.

“Tuhuma nyingine ni kupitia kampuni ya Quality Group kuhusu mapato ya klabu ya Yanga,” amesema Hamduni na alipoulizwa mahojiano hayo yatachukua siku ngapi alisema: “Suala la uchunguzi ni hatua, tutaona kadiri mahojiano yatakavyokuwa. Tulimkamata jana (juzi) uwanja wa ndege na hadi sasa tunaye.”

SOMA NA HII  KAPOMBE:- TULIFURAHIA KUPANGWA NA WASAUZI..LAZIMA TULIPIZE KISASI CHA MWAKA JANA...