Home news ULE MCHONGO WA KELVIN JOHN ‘MBAPPE’ KUJIUNGA NA KRC GENK UKO HIVI

ULE MCHONGO WA KELVIN JOHN ‘MBAPPE’ KUJIUNGA NA KRC GENK UKO HIVI


BAADA ya kuzagaa kwa tetesi kuwa, KRC Genk imempiga chini straika kinda wa Kitanzania, Kelvin John ‘Mbappe’, meneja wa kinda huyo, Mbaki Mutahaba amevunja ukimya na kufafanua kuwa kila kitu kipo freshi na wakati wowote nyota huyo anayekuja juu kitaelekewa wapi anaenda.

Mutahaba amesema straika huyo hakuwa na dili hilo la Genk tu, bali kuna wakali wengine barani Ulaya wanaomtaka Kelvin na mipango yote ipo kwenye mstari na muda mfupi ujao itawekwa wazi.

Kuzagaa kwa tetesi za kupigwa chini kwa Kelvin kulichangiwa na ukimya uliokuwa umetawala huku akionekana kuwa nyumbani kwa kipindi kirefu tangu alipotumikia taifa wakati wa mashindano ya CECAFA kwa vijana U20 yaliyofanyika Arusha na yale ya Afcon yaliyofanyika Mauritania na timu hiyo.

Lakini meneja huyo alisema sababu ya kuendelea kuwepo nchini kwa Kelvin ni marufuku iliyopo England kipindi hiki cha janga la corona hivyo kumkwamisha kurejea huko kwa sasa. Kelvin alipelekwa Brooke House FA ya England akitokea Genk ili asome na kukuzwa kisoka, lakini tangu awe nchini hajaondoka na Meneja huyo alifafanua zaidi kwa kusema; “Lengo la kumpeleka kituo cha Brooke House FA lilikuwa ni kutaka azoee kwa haraka maisha ya Ulaya, sasa alivyorudi kuichezea timu ya taifa na kupata ugumu wa kurejea England, ugumu huo ulisababishwa na uwepo wa janga la corona, kuna kizuizi kwa sasa.

“Angekuwa amesharejea lakini kwa sasa anaendelea na programu mbalimbali kwa njia ya mtandao, niwatoe shaka Watanzania kwa kuwaambia kijana yupo kwenye mikono salama na Mungu akipenda kila kitu kitakaa sawa hivi karibuni,” aliongeza Mutahaba.

Ripoti zinasema Kelvin aliyezaliwa Juni 10, 2003 akitimiza miaka 18, ataruhusiwa kikanuni kwa mujibu wa FIFA kujiunga rasmi na klabu yoyote Ulaya na hicho ndio kitu kilichoifanya hata KRC Genk kusubiri hadi kinda huyo wa Kitanzania atimize umri huo.

Licha ya kwamba wengi wanaifahamu KRC Genk kama klabu ambayo imeonyesha nia ya kutaka huduma ya kinda huyo anayetazamwa kama Mbwana Samatta mpya, wapo vigogo wengine huko barani Ulaya na wanaonekana kummezea mate, ikiwemo Lille ya Ufaransa.

SOMA NA HII  MBEYA CITY: TUNAWAHESIMU SIMBA ,TUNAZITAKA POINTI TATU

“Tumewahi kutafutwa na wawakilishi wa Lille tuliongea nao lakini hatuwezi kuweka wazi kila kitu kwa sasa, tusubiri tuone nini kitatokea, kikubwa ni kumuombea, ila Kelvin kila kitu chake kipo sawa na puuzeni hizo tetesi,” alisema.