BADO kama saa kadhaa tu kwa Simba na Yanga kuvaana katika pambano la marudiano la Ligi Kuu Bara baada ya awali kushindwa kuchezwa Mei 8, huku tambo na presha zikizidi, lakini Mtendaji Mkuu wa Msimbazi, Barbara Gonzalez amesema watani wao wajipange kwelikweli.
Barbara alisema Simba imejiandaa kubeba ndoo ya nne mfululizo ya Ligi Kuu na pia kutetea na Kombe la Shirikisho (ASFC) watakapo-kutana tena na Yanga mwishoni mwa mwezi huu mjini Kigoma.
Akizungumza ikiwa ni siku chache tangu Simba iing’oe Azam kwenye nusu fainali ya ASFC na huku chama lake lilikabiliwa na pambano la marudiano la ligi dhidi ya Yanga ukipigwa keshokutwa jijini Dar es Salaam alidai hawaachi kitu msimu huu.
“Nawapongeza wachezaji wetu na benchi la ufundi kwa kazi kubwa wanayofanya kuhakikisha timu inapata matokeo chanya. Malengo yetu kwa msimu huu ni kubeba kila kombe lililo mbele yetu na tutahakikisha tumefanya hivyo,” alisema Barbara.
Mtendaji huyo wa Simba alisema wanaanza na mechi ya Jumamosi kufanya kweli dhidi ya Yanga, kisha kuwasubiri tena kwa mchezo wa fainali ya ASFC ili kukomba mataji yote msimu huu wakiyatetea.
Mchezo wa Jumamosi wa derby ni mechi ya aina yake na kihistoria kwa timu hizo kwani endapo Simba itashinda itatangazwa kuwa bingwa, kwa vile itafikisha pointi 76, ambazo hakuna timu yoyote ya Ligi Kuu itazifikisha kwa msimu huu.
Barbara alipoulizwa kuhusu mchezo huo ambao wakishinda watakuwa mabingwa wa ligi kwa mara ya nne mfululizo alisema: “Tunatarajia kushinda, tunataka kushinda kila mechi na kila kombe, hivyo mchezo wetu wa nusu fainali ya ASFC dhidi ya Azam ulikuwa kama kupasha misuli joto kwa derby, hivyo wapinzani wetu wajiandae kupata aibu, tumepania kubeba kila kitu.
“Acha mashabiki wetu waendelee kutuombea maana safari bado ni ndefu, tulidhani msimu huu tutaumaliza Julai 18, kwenye mechi ya ligi dhidi ya Namungo, ila baada ya kushinda nusu fainali ya ASFC msimu tutaufunga rasmi Julai 25, Kigoma kwa kubeba kombe la ASFC mbele ya Yanga,” alitamba.
Endapo Simba itashinda Kigoma, itaweka rekodi ya kushinda kombe hilo kwa mara pili mfululizo