KITAUMANA! Ndivyo unavyoweza kuielezea vita kubwa kati ya safu ngumu ya ulinzi ya Yanga, dhidi ya utatu hatari wa safu ya ushambuliaji ya Simba unaoongozwa na viungo Clatous Chama, Bernard Morrison na Luis Miquissone ‘CMM’, huku Kocha wa Simba, Didier Gomes akiwapa nyota hao watatu tizi maalum la kuivunja safu ya ulinzi ya Yanga.
Katika mazoezi hayo maalum ya Simba yaliyofanyika kwenye Uwanja wa Simba Mo, Gomes alianza kwa kutenga ‘masanamu’ maalum manne kama wanavyocheza mabeki wa Yanga, halafu akawatenga viungo wake wakiongozwa na Chama, Morrison na Miquissone kuivunja safu hiyo ya ulinzi.Nyota hao walitakiwa kupiga pasi nne tu kabla ya kufika golini, na kumfunga kipa, Aishi Manula.
Pasi ya kwanza ilianzia katikati na kupigwa kwa kiungo wa kati ambaye alisimama Chama, aliyepiga pasi ya pili kuirudisha kwa kiungo wa chini aliyepiga pasi ya tatu pembeni nyuma ya masanamu ya ulinzi walipopangwa Miquissone au Morrison.
Morrison na Miquissone waliokuwa wakishambulia kutokea pembeni, walitakiwa kupiga krosi ya nne, iliyotakiwa kuunganishwa na John Bocco au Chris Mugalu waliopangwa kama washambuliaji wa kati.
Akizungumza na Championi Jumamosi, baada ya mazoezi hayo Gomes alisema: “Nimepata nafasi ya kusimamia baadhi ya dabi kubwa Afrika, hivyo najua mchezo huu una umuhimu gani kwa mashabiki, lakini naiamini timu yangu kutokana na kiwango ambacho tumekuwa nacho katika michezo yetu iliyopita.
“Tumejiandaa kwa muda mrefu na tulikuwa tunautamani mchezo huu, najua wapinzani wetu Yanga wako bora sana hasa katika eneo la ulinzi na pia wana wachezaji bora akiwemo Feisal Salum ‘Fei Toto’.“Lakini kama ambavyo nimesema, tunajiamini kuelekea mchezo huu, tuna ari kubwa kwa kuwa tuna nafasi ya kutangaza.